NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya udhibiti Usafiri Ardhini Nchini (LATRA) imetoa elimu kwa wamiliki wa Vyombo vya usafiri kuhusu umuhimu wa kuwa na umoja wao ama kampuni itakayosaidia utetezi wa maslahi yao.
Meneja wa Leseni wa Mamlaka hiyo, Leo Ngowi amebainisha hayo wakati akizungumza na wamiliki wa Daladala na Bajaji jijini Arusha leo, Januari 29, 2024 na kuweka wazi umuhimu wa wamiliki hao kuanzisha umoja ama lengo ni kuboresha huduma ya usafirishaji na wao wenyewe kujiimarisha kiuchumi.
Ngowi amesema kuwa washiriki wa semina hiyo wamepata fursa ya kujifunza mambo kadhaa ikiwemo faida ya kuwa na umoja ambao ukifanikiwa kuanzishwa utasaidia kuwa na mfumo wa kisasa ukilinganisha na mfumo wa sasa ambao unatumika bila kukidhi viwango.
Pia amesema pindi utakapoanzishwa umoja huo huduma za usafirishaji jijini Arusha zitaimairika na kuboreshwa kwa kiasi kikubwa.
Naye Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala jijini Arusha, Maulid Athuman amesema baada ya kupewa elimu hiyo amebaini kupata faida kubwa ambayo itawafanya kuwa pamoja na ameiomba Latra kuendelea kutoa elimu kwa wamiliki wote ili wapate uelewa wa pamoja.
Kwa upande wa Musa Chuga, Dereva na Mmiliki wa daladala amesema wamejifunza mambo mengi katika semina hiyo ikiwemo umuhimu wa kuwa na kampuni itakayowasimamia ama Chama cha Ushirika ambacho kitawasaidia kutatua kero au malumbano ambayo yamekua yakijitokeza baina yao na Latra na Jeshi la Polisi.




No comments:
Post a Comment