ACT WAZALENDO KUJITOA KATIKA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, March 8, 2024

ACT WAZALENDO KUJITOA KATIKA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, akizungumza na waandishi leo Machi 8, 2024 jijini Dar es Salaam.

NA MAGENDELA HAMISI

WAKATI chaguzi za Serikali za Mitaa zikitarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu kufanyika mwakani , Chama Cha ACT Wazalendo kimeibuka na kutishia kujitoa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Akizungumza leo Machi 8, 2024 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kutamatika, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kwa niaba ya ACT Wazalendo na Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi walikubaliana kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Ado amedai ACT Wazalendo waliingia katika umoja huo kwa kutoa hoja nne ambazo zilikubaliwa kufanyiwa na Rais Dkt Mwinyi ambazo ni Kuachiwa huru kwa baadhi ya wanachama wao waliokuwa wakishikiliwa kutokana na sababu za kisiasa, hoja ambayo ilitekelezwa.

Hoja nyingine tatu ambazo, Ado amedai hazijatekelezwa na Serikali ya Zanzibar ni Mageuzi ya kimfumo, Fidia kwa wahanga wa uchaguzi huo na Kuundwa kwa Tume ya Kijaji kuchunguza uvunjifu wa haki za binadamu kwenye uchaguzi huo.

“Baada ya hoja hizo tatu kushindwa kutekelezwa,  Kamati Kuu ya ACT Wazalendo kupitia kikao cha Machi 4, 2024 imetoa agizo kwa Kamati ya Uongozi Taifa, ikutanane na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar kuwaeleza kuhusu uamuzi wa chama kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa kitaifa kutokana na kutotekelezwa makubaliano hayo,” amesema..

Ameongeza kuwa waliingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuiweka Zanzibar katika hali ya amani na utulivu na si vingine kwa maana wanaipenda nchi yao na siasa isiwe sababu ya kuwaingiza katika uvinjifu wa amani.

Pia chama hicho kupitia kikao cha Halmashauri Kuu cha Machi 7 mwaka huu kimefanya chaguzi wa wajumbe wa Kamati wa Kuu wa uchaguliwa kutoka kanda 10 za chama hicho na kufanya teuzi mbalimbali ikiwemo uteuzi wa Katibu Mkuu, Ado Shaibu na manaibu katibu mkuu.

Aidha ikafanya uchaguzi wa Wajumbe wa Kamati Kuu, uteuzi wa Wajumbe wa Kamati Kuu, Wajumbe wa Halmashauri Kuu, Sekretarieti ya chama, Naibu Mwanasheria Mkuu, Wakili Bonifasia Mapunda, Idara ya Habari, Idara ya fedha, Idara ya Mambo ya Nje, Idara ya Haki za Binadamu na Idara ya Oganizeshen, Mafunzo na Uchaguzi.

No comments:

Post a Comment