ZIFF YAWATANGAZA JOSEPH MWALE, MADUDU KUWA WAKURUGENZI WAPYA WA TAMASHA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, March 18, 2024

ZIFF YAWATANGAZA JOSEPH MWALE, MADUDU KUWA WAKURUGENZI WAPYA WA TAMASHA


NA ANDREW CHALE, ZANZIBAR.

MWENYEKITI wa Bodi ya Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF), Chande Omary amewatangaza Watendaji wakuu wapya wa tamasha hilo, Bw Joseph Mwale, kama Afisa Mtendaji Mkuu mpya na Bw Hatibu Madudu kama Mkurugenzi wa Tamasha hilo.


Chande amebainisha kuwa, uteuzi wa nafasi hizo wanaanza mara moja kuanzia tarehe 15, Machi 2024 kwani ni muhimu kwa ZIFF, ukiingiza nguvu mpya na maono katika tamasha hilo lenye umri wa miaka 26. 


Aidha, amesema kuwa, ni baraka ya kipekee kuwapata Vijana hao Wazalendo katika kuendesha tamasha hilo kongwe, katika kufikia umri mkubwa wa tamasha kwani watalifikisha mbali zaidi.


Nae Prof Martin Mhando, Mkurugenzi wa Tamasha anayemaliza muda wake, amesema; "Uongozi huu wenye nguvu ya ujana ndio dawa inayohitajika ili kulifufua tamasha." Amebainisha.


Aidha, amebainisha kuwa, Joseph Mwale anatimiza miaka 15, akianzia kama mkufunzi wa ZIFF hadi kuwa Meneja Masoko wa ZIFF na sasa ni Mzanzibari wa kwanza kuongoza ZIFF. 


Kwa upande wake, Madudu ni mtengenezaji wa filamu ambaye ameshinda tuzo za kimataifa na katika ZIFF amekuwa Mkurugenzi msaidizi wa Tamasha la ZIFF mwaka jana akijifunza kutoka kwa Mkurugenzi mkongwe, Profesa Mhando.


“Tamasha liko katika mikono mizuri  ya watu wenye uzoefu wa ZIFF. Timu inaleta maono mapya yanayoendana kikamilifu na kauli mbiu ya ZIFF ya 2024 ya “Kuhuisha”.


Watahamasisha kila mtu kuungana na kuifikisha ZIFF katika viwango vipya." Amesema Thani Mfamau, Makamu Mwenyekiti wa ZIFF.


Nae Mkurugenzi mpya wa Tamasha Hatibu Madudu amesema; "Tunahitaji kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kuwawezesha watengenezaji filamu wa nchi zote kutumia jukwaa la ZIFF kuendeleza tasnia ya filamu Afrika." 


ZIFF imekuwa na mchango mkubwa katika kuangazia ukuaji wa filamu za humu nchini kwa miaka mingi na imehamasisha filamu bora zinazozalishwa nchini Tanzania.


Katika kipindi cha miaka 3 iliyopita filamu zilizoongozwa na kutayarishwa na Watanzania zimeshinda filamu bora zaidi katika ZIFF ambapo Mwaka 2021 ilikuwa Binti ya Seko Shamte, 2022 ilikuwa Vuta N’Kuvute ya Amil Shivji na mwaka jana ilikuwa Eonii ya Eddie Mzale.


..Filamu hizi zote zimeendelea kuonyeshwa kimataifa na kuuzwa kwa masoko kama Netflix, na Eoniii ina onyeshwa kwenye ndege za Emirates, kukiri ubora wa filamu hizi za Kitanzania.


Aidha, ametoa wito kwa wafadhili wa ndani kuunga mkono ZIFF ilikuongeza utangazaji wa filamu za Zanzibar katika jukwaa hilo.


Tamasha hilo la ZIFF, limekuwa likifanyika katika Mji Mkongwe Unguja Visiwani hapa huku matukio ya Sanaa na tamaduni tajiri za Bara la Afrika, India, Pakistan, Mataifa ya Ghuba, Iran na visiwa vya Bahari ya Hindi, hujumuisha mashindano ya kimataifa ya filamu, muziki, ukumbi wa michezo, sanaa za maonyesho, warsha, semina, makongamano, na sanaa 



mbali mbali.

No comments:

Post a Comment