Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati Tendaji ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) akisisitiza jambo katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Jijini Dar es Salaam jana.
NA MWANDIHI WETU
SERIKALI imepongezwa utekelezaji wa
mapendekezo ya sekta binafsi kupitia vikao na mikutano ya Baraza la Taifa la
Biashara (TNBC) ambapo sekta binafsi imekiri kupatikana kwa mafanikio makubwa
Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) ndani ya kipindi
cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mara baada ya kikao cha 37 cha
Kamati Tendaji cha TNBC jana, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Dkt. Moses Kusiluka amesema sekta binafsi imeridhishwa na hatua
mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha na
kuweka mazingira na wezeshi ya uwezeshaji na ufanyaji biashara hapa nchini.
“Ni faraja kwetu kupata mrejesho chanya kutoka
sekta binafsi kwani inaleta afya na inaonesha dhamira ya kweli kuwa
Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuleta mageuzi ya kiuchumi pamoja na
kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji,” amesema Dkt.
Kusilluka.
Mwenyekiti huyo wa kamati tendaji amesema Serikali
imeshaondoa tozo mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa ustawi na ukuaji wa
biashara hapa nchini kwa hayo yote ni matunda ya kazi ya Baraza la Taifa la
Biashara.
Aidha, Dkt. Kusiluka amelipongeza Baraza kwa
kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo kusimamia na kuhakikisha vikundi kazi vyake
ambavyo makatibu wakuu ndiyo wenyeviti wa vikundi kazi hivyo.
Amesema vikundi kazi vimefanya kazi nzuri
ikiwemo kujadiliana na hatimaye kuja na mapendekezo
yanayowasilishwa kwenye kikao cha kamati tendaji kabla ya
kupelekwa kwenye mkutano wa Baraza mwishoni mwa mwezi Mei au Juni
mwanzoni ambapo Rais ndiye mwenyekiti wake.
“Miaka mitatu ya uongozi wa Awamu ya Sita
chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
imeweza kuboresha na kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara
na uwekezaji nchini ikiwemo kuchochea ukuaji wa sekta binafsi,” amesema
Dkt. Kusiluka.
Naye Mwenyekiti Mwenza ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini (TPSF), Angelina Ngalula ameipongeza Serikali
kwa kufanya maboresho makubwa na kufanikishwa utekelezaji Mkumbi.
”Serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu zaidi
kwa umma na wadau mbalimbali ili waweze kuelewa namna Mpango wa Kuboresha
Mazingira ya Biashara (Mkumbi) unavyofanya kazi kwani utasaidia kuondoa
mkanganyiko baina ya wafanyabiashara na sekta ya umma,” amesisitiza Ngalula.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt
Godwill Wanga amesema kikao hicho kimeangazia zaidi utekelezaji wa maazimio ya
kikao cha 36 cha kamati tendaji ambapo jitihada kubwa zimechukuliwa katika
utekelazaji wa maazimio hayo yenye lengo la kuboresha mazingira ya ufanyaji
biashara nchini.
Aidha Dkt. Wanga amesema moja ya
ajenda kubwa iliyojadiliwa ni pamoja na kuunganisha mifumo
ya Serikali ili weze kusomana na hivyo kujenga uchumi wa kidijiti
utakao chochea na kuongeza tija katika uzalishaji na utoaji huduma
nchini.
“Mapinduzi ya uchumi wa kidijiti
utatoa mchango mkubwa katika kukuza pato la mwananchi mmoja
mmoja na taifa kiujumla sambamba na kuchagiza maendeleo na ukuaji wa sekta
nyingine za maendeleo na uchumi,” amesema Dkt Wanga.
Dkt. Wanga amesema kikao hiko
kimeelekeza masuala yote ya udhibiti yahakikishe yanadhibiti zaidi changamoto
kuliko kuwadhibiti wazalishaji ili kutoathiri ukuaji wa uchumi sambamba
na kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ili iweze
kuzalisha na kuchangia kikamilifu katika kukuza pato la Taifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Abasi Hassan (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa (Kushoto) wakimfuatilia Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati Tendaji ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) wakati kikao cha kamati Tendaji kilichofanyika Jijini Dar es Salaam jana.
No comments:
Post a Comment