SWISSAID TANZANIA YAISHAURI SERIKALI KUWEKEZA KWENYE KILIMO HAI ILI KUZALISHA MAZAO SAFI NA SALAMA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, April 20, 2024

SWISSAID TANZANIA YAISHAURI SERIKALI KUWEKEZA KWENYE KILIMO HAI ILI KUZALISHA MAZAO SAFI NA SALAMA


 NA SELEMANI MSUYA

SHIRIKA la SwissAid Tanzania limesema ili nchi kuwa na kizazi chenye afya na ardhi bora inayofaa kwa kilimo kwa siku zijazo ni muhimu kuwekeza katika kilimo hai ambacho kinazalisha mazao safi na salama.


Aidha, SwissAid imeshauri serikali kutoa mafunzo ya kilimo hai au ikolojia kwa vijana wanaoshiriki Program ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa SwissAid Tanzania, Betty Malaki wakati akizungumza na waandishi wa habari katika shamba la mfano linalozalisha mazao kwa njia ya kilimo hai, lililopo katika Kituo cha Kilimo cha Bihawana mkoani Dodoma.


Amesema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha matumizi ya viautilifu vyenye kemikali kwenye kilimo, hali ambayo inachangia ardhi kuchoka na watu kupata madhara, hivyo njia pekee ya kuponya ardhi na watu ni kilimo hai.


Amesema SwissAid imekuwa ikitelekeza miradi ya kilimo hai mkoani Lindi, Pwani, Morogoro na Mtwara ambapo mwitikio umekuwa mzuri, jambo ambalo limewasukuma kuongeza kampeni ya kilimo hicho hadi Dodoma.


Malaki amesema mkoa wa Dodoma ambao ni mkame wanatekeleza mradi wa shamba la mfano katika Kituo cha Bihawana na matokeo yake yamekuwa mazuri.


“Sisi SwissAid tumekuwa tukipigania kilimo hai kwa kuwa ni salama kwa mkulima, mlaji na ardhi, tofauti na kilimo cha kisasa kinachotumia viuatilifu vyenye kemikali zizoathiri watumiaji na  ardhi,” amesema.


Mkurugenzi huyo amesema matamanio yao ni kuona wakulima wote Tanzania wanajua kuzalisha mazao yao kwa njia ya kilimo hai kwa kuwa kimeonesha faida kubwa zaidi ya kilimo cha kisasa.


“Ili tuweze kupata kizazi kijacho chenye afya na kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni lazima tuwekeze kwenye kilimo hai na mradi huu wa Bihawana tunautumia kama eneo sahihi la kuthibitisha kwamba kilimo hiki kinawezekana,” amesema.


Kwa upande mwingine Malaki ameishauri Serikali kutoa elimu ya kilimo hai kwa vijana ambao wanashiriki kwenye program ya BBT ili waweze kuchagua upande sahihi.


Ofisa Program wa SwissAid anayesimamia Utafiti na Utetezi wa Kilimo Hai, Gladness Martin amesema shamba la mfano lililopo Bihawana limeonesha matokeo chanya hali ambayo imetoa msukumo kwao kupigania kilimo hicho.


Martin amesema pamoja na mafanikio makubwa ambayo yameonekana kupitia shamba hilo, bado serikali haijaonesha nia ya dhati ya kuunga mkono jitihada hizo, hivyo kuiomba iangalie eneo hilo kwa jicho la upendeleo.


Amesema pamoja na changamoto ya ukame mkoani Dodoma kilimo hicho kimeweza kufanyika kwa ubora, hivyo anaomba wakulima wa Tanzania kujikita katika kilimo hai.


“Kilimo hiki kinahitaji mbolea ya mifugo na nyingine za asili ambazo tumepanda hapa shambani. Kwa lugha ya mjini naweza kusema mbolea ya mazao inapatikana shambani na ni salama kwa afya zetu,” amesema.


Ofisa huyo amesema katika shamba hilo la mfano wamezalisha mbogamboga, nyanya, matango, miti ya kuhifadhi shamba, mkuna ambao ni mbolea na mengine mengi.


Mwenyekiti wa Mwavuli wa Asasi za Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM),, Dk Mwatima Juma amesema ili kilimo hai kiweze kupiga hatua ni lazima kuwepo utashi wa kisiasa jambo ambalo kwa sasa halipo.


Dk Mwatima amesema kitendo cha kuhamasisha kilimo cha kisasa ambacho kinatumia viuatilifu ni sawa na kurejea utumwani na madhara yake yamekuwa yakionekana kila kukicha.


Amesema kasi yakuongezeka magonjwa hasa yasiyoambukiza inatokana na matumizi ya vyakula vyenye kuzalishwa kwa viuatilifu vyenye kemikali mbaya.


“Inahitajika utashi wa kisiasa kuhakikisha kilimo hai kinapiga hatua, tuachane na kufanya kilimo biashara, tunamaliza watu wetu kiuchumi na kiafya, kwani ni wazi soko la mazao ya kemikali halipo duniani,” amesema.


Mwenyekiti huyo amesema kwa hali ilivyo sasa hakuna haja ya kupigania wizara ya kilimo iongozewe bajeti, kwani bajeti hiyo inanufaisha wazalishaji wa pembejeo zenye kemikali, huku kilimo hai kikipuuzwa.


Mratibu wa Kilimo Ikolojia Tanzania, Mujuni Mtembei amesema Serikali inatambua faida za kilimo hai na kwamba inaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na Kikosi Kazi cha Mbegu za Wakulima.


“Serikali haiwezi kubagua aina ya mbegu au kilimo, nikuhakikishie sisi kama wizara tunatambua faida za kilimo ikolojia ndio maana leo ninasimamia eneo hilo, nawaomba wadau wote watambue kuwa tupo pamoja na hakuna upendeleo wowote,” amesema.







No comments:

Post a Comment