SERIKALI KUNUNUA MITAMBO KUMI (10) YA UCHORONGAJI KWA AJILI YA WACHIMBAJI WADOGO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, May 18, 2024

SERIKALI KUNUNUA MITAMBO KUMI (10) YA UCHORONGAJI KWA AJILI YA WACHIMBAJI WADOGO


NA MWANDISHI WETU

SEEIKALI kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imepanga kununua mitambo mingine 10 ya uchorongaji kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo nchini.


Hayo yamesemwa 17 Mei, 2024 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde aliposhiriki zoezi la kuwakabidhi leseni Chama cha Wanawake Wachimbaji Mkoani Simiyu (TAWOMA) katika Kata ya Dutwa Wilayani Bariadi.


"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha za kuongeza mitambo mingine 10 ya uchorongaji kupitia STAMICO na ametuelekeza kuwa mitambo hiyo ikifika nchini Mwezi Agosti au Septemba, 2024 mitambo 2 tuiweke mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo wanawake na vijana" amesema Waziri Mavunde 


Ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwawezesha wachimbaji madogo kwa kuwapatia vifaa na kuimarisha shughuli zao ili ziwanufaishe watanzania.


Aidha, Waziri Mavunde amemwagiza Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Simiyu, Bw. Mayigi  Makolobela kusimamia vijana na wanawake ili waunde vikundi, ili katika maeneo yanayorejeshwa Serikalini kwa zoezi la ufutaji wa leseni vikundi hivyo vipatiwe maeneo ya uchimbaji.


Akisoma risala kwa niaba ya Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake (TAWOMA), Mwenyekiti wa TAWOMA Taifa, Bi. Semeni Malale ameishukuru Serikali kwa namna inavyoendelea kuwawezesha wachimbaji wanawake nchini kuendesha shughuli zao na pia kumshukuru Ndg Emmanuel Silanga”Gungu” kwa kutoa Leseni hiyo kwa wakina mama wa Mkoa wa Simiyu.


Pia, pamoja na mambo mengine, Bi. Semeni ametoa wito kwa wanawake wenzake kuchangamkia fursa hiyo ya uchimbaji baada ya kupokea leseni hiyo, huku akiiomba Serikali kuendelea kusaidia baadhi ya changamoto katika eneo la uchimbaji la Dutwa ikiwemo maji na barabara.


Naye, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda ameishukuru Serikali kwa namna inavyosimamia sekta ya madini, na kuahidi kwamba ataendelea kutoa ushirikiano kwa akina mama na vijana wachimbaji madini ili shughuli zao ziendelee kuwanufaisha na kuchangia katika ustawi wa uchumi wa Mkoa wa Simiyu.


Akijibu changamoto za TAWOMA katika eneo la Dutwa, Dkt. Nawanda amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Simon Simalenga kuhakikisha anasimamia suala la kuboresha barabara na kuleta maji katika eneo hilo la uchimbaji, kwani Serikali imeshaleta zaidi ya bilioni 4 Mkoani Simiyu kwa ajili ya uboreshaji barabara na mtandao wa maji.







No comments:

Post a Comment