NA MAGENDELA HAMISI
WAKALA wa Shirika la Meli Tanzania (TASAC) imekabidhiwa boti mpya ya doria aina ya BP SAILFISH na Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa ajili ya kuimalisha ulinzi katika Bahari Kuu na Maziwa Makuu pamoja na kukabiliana na vitendo vya kihalifu nchini.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt Jimmy Yonazi, amesema boti hiyo imenunuliwa kupitia mradi wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari Kuu na Maziwa Makuu nchini kwa ufadhiri wa Serikali ya Japani na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Dkt Yonazi amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya kuikabidhi boti hiyo kwa TASAC na akasisitiza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ina imani kubwa na uwezo wa Tasac katika kusimamia, kutunza na kuboresha mazingira ya boti hiyo.
"Lengo kuu la kukabidhi boti hii ni kuimalisha doria na kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu, hivyo nitoe wito kwa TASAC kuitunza ili idumu kwa muda mrefu na itimize lengo lililokusudiwa," amesema.
Aidha ameongeza kuwa lengo la misingi ya boti hiyo ni kuimalisha doria, ulinzi na usalama katika mipaka ya nchi yetu.na doria hizo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya Tanzania za kukabialiana na vitendo vya kihalifu kama vile uvuvi haramu, uhamiaji haramu, usafirishaji wa dawa za kulevya, biashara za magendo na utoroshwaji wa nyara za Serikali
Pia ameiomba TASAC kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Idara ya Menejimenti ya Maafa, iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kuweza kuratibu programu za uokozi kwa majanga ya majini na usalama wa bahari kwa ujumla.
Akasisitizia kuwa matumizi ya boti hiyo yazingatie mwongozo wa kitaifa wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu wa mwaka 2022.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salim, amesema kwamba Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa ili kuimalisha ulinzi na usalama wa usafiri wa majini, hivyo kukabidhiwa boti hiyo ni hatua muhimu ya kuimalisha ulinzi na usalama katika usafiri wa majini.
"Boti hii itatuwezesha kuimalisha ulinzi dhidi ya shughuli haramu zinazoendelea kuripotiwa katika maeneo ya Bahari na Maziwa Makuu ambayo yanahitaji mikakati ya udhibiti wa shughuli hizo.
"Hivyo tunaishukuru Serikali yetu kwa kuendelea kupambana na matukio haramu na ya kihalifu," amesema.
Ameongeza kuwa bodi hiyo itasaidia utekelezaji wa majukumu ya TASAC yanayosimamiwa na sheria, hususan jukumu la usimamizi wa usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira dhidi ya uchafuzi utokanao na shughuli za meli.
Pia Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi, Ludovick Nduhiye amesema kwamba hiyo kumekuwa chachu katika kutimiza dira inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye huduma za uchukuzi na hali ya hewa zenye uhakika na salama nafuu.
"Pia itakuwa jibu katika utekelezaji wa mlengo na jitihada zinazofanywa na Wizara ya Uchukuzi kwa kushiriana na vyombo vya dora pamoja na wadau wengine wa sekta ndogo ya usafiri majini katika kudhibiti vitendo vya kihalifu katika maeneo ya mwambao wa Bahari na Maziwa Makuu," amesema
![]() |
No comments:
Post a Comment