4R ZAVUTIA VYAMA KUSHIRIKI UCHAGUZI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, October 7, 2024

4R ZAVUTIA VYAMA KUSHIRIKI UCHAGUZI


NA SELEMANI MSUYA


VIONGOZI wa Vyama vya CHAUMA, UPDP, CCK na ACT Wazalendo wamesema wamejipanga kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, kwa kile walichodai kuridhishwa na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan unatumia falsafa ya 4R.


Falsafa ya 4R ya Rais Samia imejikita kwenye Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya.


Wakizungumza ofisini kwao baada ya kumpokea Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, viongozi hao vyama wamesema walikuwa wameshakata tamaa ya kushiriki chaguzi ila kupitia uongozi wa Rais Samia watashiriki na kuibuka na ushindi.


Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi (CHAUMA), Hashimu Rungwe amesema wanaimani na uongozi wa Rais Samia katika kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo wamejipanga kushiriki kwa nguvu zote kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kuikomboa nchi.


"Tumemaliza uchaguzi wa ndani ya chama, tunajipanga kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwani 4R za Rais Samia zimetoa mwanga wa kisiasa. Tunaenda kushindana na kwa sera yetu ya ubwabwa na ustawi wa kijinsia tunaenda kufanya vizuri," amesema.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojole amesema kinaenda kushiriki uchaguzi huo kwa kuwa wanaona nchi inaendeshwa kwa amani na umoja.


Mwaijojole alitumia fursa hiyo kumuomba Waziri Lukuvi kufikisha ujumbe kwa Rais Samia kuwa vyama vya siasa vinaomba kupata ruzuku ili viweze kuleta ushindani sawa wa kisiasa nchini.

"Sisi tutashiriki uchaguzi kwani 4R zimetubutia, hatuhitaji kuandamana kwa sasa tunaenda kuleta ushindani wa kisiasa huko mitaa," amesema.


Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema chama chao kimejipanga kushinda uchaguzi huo na kumuomba Waziri Lukuvi kuelekeza wanasiasa na watendaji wakorofi kuacha kuharibu uchaguzi.


"Sisi tupo kazini kutoa elimu kwa wananchi kujitokeza kupiga kura na hasa kukichagua chama chetu, ila kuna changamoto za baadhi ya wanasiasa na watendaji ambao wanashindwa kuenzi 4R za Rais Samia waambie wabadilike," amesema.


Semu alisema uthubutu wa Waziri Lukuvi  kutembelea vyama vya siasa ni ishara njema ya kupelekwa kwenye chaguzi za haki na kidemokrasia.


Naye Mwenyekiti wa Chama cha UPDP,  Twalib Kadege amesema ziara ya Waziri Lukuvi imefungua kurasa mpya katika siasa za Tanzania huku akiahidi chama chake kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unafanyika mwezi ujao.


Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake kwa siku ya leo, Waziri Lukuvi amewahakikishia na kuwatoa hofu wananchi kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani utazingatia  kanuni na sheria hivyo kila mtu anatakiwa kushiriki kikamilifu.



Hivyo alivitaka vyama vyote vyenye usajili wa kudumu nchini kuwahimiza wanachama wao kushiriki uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na kupiga kura siku ya uchaguzi.


 

Waziri Lukuvi ambaye yupo kwenye ziara ya kutembelea vyama 19 vyenye usajili wa kudumu amesema lengo la kutembelea vyama hivyo ni kujitambulisha ofisi za chama hicho sehemu zilipo.


Waziri Lukuvi aliviambia vyama hivyo kuwa vitisho vya watu sio vya Serikali ila serikali inataka siasa zenye tija ambazo  zitawaletea manufaa wananchi.


“Nawaondoa hofu wananchi kinachotakiwa siku ya kupiga kura nendeni mkapige kura na wakati wa kampeni hakikisheni mnasikiliza kwa makini sera na hoja kwa chama husika,”amesema Waziri Lukuvi.


Hata hivyo Waziri Lukuvi alivitaka vyama hivyo kutumia falsafa ya 4R ya Rais  Samia ambayo imeonesha matunda katika kuendesha nchi.


“Ingependeza zaidi vyama vyote vya siasa vishindane kwa sera na hoja ili wananchi wapate nafasi nzuri ya kuwachambua na kujua ni nani wa kumpigia kura,”alisema.


Hata hivyo Waziri Lukuvi alivihakikishia vyama hivyo kuwa dhamira ya Rais Dk.Samia ni kuona chaguzi zote zitakazofanyika chini ya utawala zinakuwa huru na haki.


“Msidanganyike wananchi chaguzi zote zijazo zitakuwa huru na haki chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,”alisema


Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema Waziri Lukuvi amekuja na utaratibu mpya na mzuri ambao unaonesha kuviweka pamoja vyama vya siasa.


Jaji Mutungi amesema anavishukuru vyama vyote 19 vyenye usajili wa kudumu ambavyo vimeonesha nia ya kukutana na Waziri.


“Utaratibu ulioanzishwa na Waziri Lukuvi ni mzuri na unaonesha utawajenga wanasiasa kuwa wamoja kwa lengo la kujenga nchi yetu,”amesema Jaji Mutungi.


Jaji Mutungi amesema ziara iliyofanywa na Waziri Lukuvi inamanufaa mbalimbali ikiwemo kujua zilipo ofisi za vyama hivyo.


No comments:

Post a Comment