MVUA ZA VULI ZITAKUWA ZA WASTANI - TMA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, October 31, 2024

MVUA ZA VULI ZITAKUWA ZA WASTANI - TMA


NA MWANDISHI WETU


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli ambazo tayari zimeanza kunyeesha katika mikoa mbalimbali nchini.


Akitangaza mwelekeo huo leo Oktoba 31, 2024 Kaimu Mkurugenzi wa TMA,  Ladislaus Chang'a amesema katika kipindi cha Novemba 2024 hadi April 2025 mvua za vuli zitakuwa za wastani katika baadhi ya maeneo nchini.


Amefafanua kwamba kuanzia Novemba hadi Desemba 2024 mikoa ambayo inapata mvua msimu miwili kwa mwaka ikiwemo Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, na Dar es Salaam.

 Pia amesema mikoa ya Kaskazini ya Mkoa wa Morogoro, Pwani pamoja na visiwa vya Mafia na Zanzibar ambao utabiri wake ulitolewa   Agosti 22,  2024 ambayo  mvua za wastani zinatarajiwa


DK Chang'a amesema kwamba mvua za chini ya wastani hadi wastani zilitarajiwa kuwepo katika  maeneo mengi ya Pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki. 

Pia katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria mvua zilitarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani. 

Wakati huo huo amebainisha kwa msimu wa Vuli, 2024 ulitarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha.
 
Aidha, mvua hizo zilitarajiwa kuanza kwa kusuasua wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2024 katika ukanda wa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine yanayopata mvua za Vuli kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Oktoba, 2024. 

Mvua hizo tayari zimeanza katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria na pwani ya kaskazini kama ilivyotabiriwa. Hata hivyo, maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki yameendelea kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu. 


Aidha, amefafanua kuwa utabiri wa mvua za Vuli unatarajiwa kuendelea kama ulivyotabiriwa ambapo mwelekeo wa mvua za Msimu wa Novemba, 2024 hadi Aprili, 2025, Mvua hizo ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro. 

"Maeneo haya yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, unaoanza Novemba na kuisha kati ya Aprili na Mei 2025.


"Kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa kuwa mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma; kaskazini na mashariki mwa mkoa wa Lindi, na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa" amesema

 "Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya kusini na magharibi mwa mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro." amesema.

Aidha amesema mvua nyingi zinatarajiwa katika kipindi cha nusu ya pili ya msimu kuanzia Februari – Aprili, 2025 ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya Mwezi Novemba, 2024 hadi Januari 2025.

Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi wa TMA amesema kuwa Mifugo na Uvuvi katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, wafugaji na wavuvi wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho, maji na chakula cha samaki. 

Hata hivyo amesema milipuko ya magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa wa miguu na midomo, na kuzaliana kwa wadudu wadhurifu kunaweza kujitokeza. 

Pia amesema upungufu wa mvua hasa katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2024 hadi Januari, 2025) unatarajiwa kuathiri upatikanaji wa maji na malisho ya mifugo na kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.


No comments:

Post a Comment