NA
MAGENDELA HAMISI
OFISI
ya Takwimu (NBS) imesema tasnia ya takwimu ni kama nyingine hivyo ni vema
ikaeshimiwa na kusisitiza kwamba taarifa ambazo zimetolewa na Serikali kuhusu
idadi ya watu ambao wamejiandikisha kupiga kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa
2024 ni sahihi.
Dkt
Albina Chuwa amefafanua hayo leo Oktoba 28, jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku
chache kupita baadhi ya watu kujitokeza kupitia mitandao ya kijamii kupotosha
umma taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa kuhusu matokeo ya zoezi la uandikishaji
wapiga kura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka
huu.
“Tasnia
ya takwimu ieshimiwe kwani ni sawa na nyingine kama udaktari, hivyo kupotosha
taarifa zilizotolewa na Serikali ni kosa kisheria nataka kuwaambia wananchi
ambao wamejiandikisha kwa ajili ya katika uchaguzi huo ni 31,282,331 sawa na
asilimia 94.83 ya watu wote wenye umri wa kujiandikisha kwa mwaka 2024.
“Takwimu ambazo wao
wanazizungumzia watu hao ni takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na
ulinganishaji wanaoufanya hauendani na hali halisi ya idadi ya watu wenye sifa
za kujiandikisha kupiga kura mwaka huu, amesema.
Amefafanua kwamba kwa hesabu za kawaida idadi ya watu nchini kwa mwaka 2022
haiwezi kulingana na idadi ya watu kwa mwaka 2024 kwani hivi sasa tayari miaka
miwili kamili imeshapita tangu imkufanyika kwa sensa hiyo.
Amesema kutokana na makadirio ya idadi ya watu kwa 2024, idadi ya watu nchini
inakadiriwa kuwa Milioni 66.3 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 3.2 kwa
mwaka kama ilivyopatikana kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
“Makadirio haya kwa Tanzania Bara yanakadiriwa kufikia watu milioni 64.2 na kwa
Tanzania Zanzibar yanakadiriwa kufikia watu milioni 2.03, kwa makadirio haya,
wananchi tunapaswa kufahamu kuwa idadi ya watu kwa mwaka 2024 haiwezi kuwa
sawasawa na ile ya mwaka 2022,” amesema.
Dkt. Chuwa amesema watu waliokuwa na umri wa miaka 16, 17 na 18 katika Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2022 hivi sasa wana umri wa miaka 18, 19 na 20 ambao
idadi yao ni 3,785,036 waliokidhi kigezo cha umri wa kujiandikisha kupiga kura
katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka huu kwa kuwa wana vigezo na sifa za
kupiga kura.
Amesema idadi ya watu wenye umri wa kupiga kura ni sawa na watu wote ambao
mwaka 2022 walikuwa na umri wa miaka 16 na zaidi ama kwa lugha nyingine ni wote
ambao ifikapo Novemba 27, mwaka huu, watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 au
zaidi.
“Kwa hesabu hiyo inatokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022,
makadirio ya idadi hiyo ya watu wenye umri wa kupiga kura katika uchaguzi wa
Serikali za Mitaa ambayo ni watu 32,987,579 ni sahihi na ni rasmi kulingana na
Kanunuzi za Msingi za Umoja wa Mataifa Kuhusu Takwimu Rasmi na kama
ilivyoripotiwa kwenye taarifa ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI,”
amesema.
Dkt.Albina amesema kuhusu kiwango cha uandikishaji kwa mikoa, imejitokeza
baadhi yake kuwa na asilimia zaidi ya 100 ya watu walioandikishwa na kufafanua
kuwa watu wana tabia ya kuhamahama kutoka eneo moja kwenda eneo na kusababisha
uandikishaji wa watu wengi zaidi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka
2022 kwa baadhi ya mikoa.
“Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ilihesabu watu kulingana na mahali
walipolala usiku wa kuamkia siku ya Sensa yaani Agosti 23, 2022. Kwa hivyo,
hili ni jambo la kawaida na linalowezekana kutokea kama ilivyotokea katika
mikoa hiyo ya Pwani (asilimia 112.61); Tanga (asilimia 110.82); Mwanza
(asilimia 106.58); Dodoma (asilmia 104.19) na Iringa (asilimia 100.54),”
amesema.
Amesema idadi kubwa ya watu mkoa wa Pwani inatokana na watu wengi wa Dar es
Salaam kuwa na makazi mkoa wa Pwani hasa katika wilaya za Bagamoyo, Kibaha,
Kisarawe na Mkuranga. Kwa hiyo ongezeko hilo la watu kwenye maeneo hayo
linachangiwa na kuhama kwa watu na si kwa kuandikisha watu waliokosa sifa.
Mikoa yenye asilimia ndogo ya uandikishaji ni ile ambayo chambuzi za kitakwimu
zinaonesha ni mikoa yenye uhamaji mkubwa wa watu kwenda katika majiji.
Dk. Albina alitoa takwimu za sensa kwa makundi ya umri na kulingana na Sensa ya
Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watoto walio na umri chini ya miaka 15
nchini ilikuwa 26,399,989 sawa na asilimia 42.8.
Pia idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi wenye umri miaka 15 hadi 64
walikuwa 33,000,128 sawa na asilimia 53.4 na idadi ya wazee walikuwa 2,341,003
sawa na asilimia 3.8.
Amesema wastani wa watoto chini ya umri wa miaka 15 kuwa ni asilimia 60 hadi 70
ni upotoshaji mkubwa kwani hata viwango vya Afrika, asilimia ya watoto ni kati
ya asilimia 40 hadi 45 na si vinginevyo.
“Hizi ndizo takwimu rasmi za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa mujibu
wa Sheria ya Takwimu sura 351 kwa maana hiyo, taarifa iliyotolewa na Serikali
ya Idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi ujao wa Serikali
za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024 ni sahihi kwa sababu kiujumla
idadi ya watu wote waliojiandikisha nchini haijavuka ile inayotokana na matokeo
ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022,” amesema
Amesema takwimu hizo hazina mashaka yoyote na kuonya kutopotosha umma kwani ni
kosa kisheria kupotosha umma kwa kutumia takwimu rasmi kwa mujibu wa Sheria ya
Takwimu.
Naye Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara, Spika Mstaafu Anne
Makinda aliwataka Watanzania kuacha upotoshaji kwani takwimu zilizopo ni sahihi
na zimefuata vigezo vyote.
“Hii ndio taarifa rasmi, takwimu za sensa ndio msingi wa kufanyia kitu kama
zisingekuwepo tusingepata asilimia, takwimu za sensa ni mwongozo wa kufanya
mambo yote ya maendeleo,” amesema.
No comments:
Post a Comment