![]() |
NA MAGENDELA HAMISI
VIKUNDI vya Wanawake na Vijana wanaojihusisha na kilimo cha mwani wamekabidhiwa vifaa zinazotumika ikiwemo mashine ya kukoboa na nyinginezo kwa lengo la kuwaongezea uwezo wa uchakati zao ili kufikia mafanikio katika uchumi wa buluu.
Vifaa hivyo vimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Serikali kupitia Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa 'Maisha Bahari'.
Mradi huo unatekelezwa na Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijni, kwa lengo la kuhamisisha na kuendeleza agenda ya kimataifa ya Uchumi wa Buluu na Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayopiga hatua kubwa katika uchumi wa buluu kupitia kilimo cha mwani.
Wakati akikabidhi vifaa hivyo, kwa wakulima wa mwani ambao wamefika jijini Dar es Salaam wakitokea mikoa ya kimkakati kwa kilimo hicho ili kunuia uchumi wa buluu, Mkurunzi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara, amaefafanua kwamba wataendelea kutoa msaada kama huo kwa vikundi hivyo ili kukuza uchumi wa buluu kupitia kilimo hicho.
"Tutaendelea kutoa misaada ya aina hii ikiwa vifaa kama hivi ili kwenda sanjari na utekelezaji wa agenda ya kimataifa ya uchumi wa bluu,Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa kwenye uchumi wa bluu katika sekta ya mwani na tunaamini thamani ya zao hili itapanda na kukuza kipato cha mkulima na taifa kwa ujumla "amesema.
Pia Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt Edwin Mhede amesema suala la kuchagiza maendeleo ya Uvuvi na Kilimo cha mwani ni utekelezaji wa azimio namba 14 la maendeleo endelevu ya Dunia na ifikapo mwaka 2030 ni dhahiri tutakuwa tumepiga hatua kubwa na azimio hilo limezungumzia suala la maisha chini ya maji .
"Nakipongeza Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa kuwa mstari wa mbele kuchagiza na kuwa sehemu ya kutoa mafunzo kwa wakulima wetu ili kuhakikisha wanapata ufahamu wa matumizi sahihi ya teknolojia ili kuongeza thamani ya mwani na kukuza kipato cha wakulima hawa"amesema Dkt Mhede
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt Batrida Buriani kwa upande wake amesema mkoa huo una rasirimali nyingi za bahari na kutokana na hilo umekuwa ukitoa sisitiza kuhakikisha wanaimarisha usalama kwenye shughuli za uvuvi pamoja na kilimo cha mwani.
Ameongeza kuwa mkoa huo kwa sasa una wakulima wa mwani wapatao 5,000 na vikundi 20 vya wanenepeshaji wa kaa, pamoja na wafugaji wa jongoo bahari jambo ambalo anaamini watafanya vema katika kuinua na kupata mafanikio kupitia uchumi wa buluu.
"Kitu tunachokifanya leo ni jambo ambalo linaweza kuchochea shughuli zetu za uchumi wa bluu,tunaona kuna fursa kubwa katika kilimo hiki japo tumeanza kwa kuchelewa wenzetu wa Zanzibar walitangulia mapema katika kilimo hiki ingawa nasi naamini licha ya kuchelewa tunafanya vizuri", amesema.
Dkt Buriani ameweka wazi kwamba Mkoa wa Tanga, wamekipokea kilimo hicho na wanafursa kubwa ya kubwa vizuri kwa kuwa kunaeneo la bahari lenye ukubwa wa kilometa 180 na kikubwa kinachotakiwa ni kupeana mbinu za uwezeshaji imara za kuhakikisha wanafikia mafanikio.
"Kwa hakika tunawashukuru UNDP kwa uwezeshaji huu walioufanya,kwanza wametoa mafunzo ya wakulima wetu wa mwani na vikundi mbalimbali kwa Mkoa wa Tanga zaidi ya wakulima 50 wamepata mafunzo sambamba na mashine za kusaga na kukausha mwani pamoja na kamba na Taitai "amesema
Naye Mkurugenzi wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kanda ya Ziwa, Profesa Juvenal Nkonoki ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo hicho amesema, Mradi wa Bahari Maisha ni sehemu ya juhudi za kusaidia jamii za Pwani kupitia kilimo cha mwani, ufugaji wa kaa, na ufugaji wa jongoo bahari.
"Kutokana na kutambua umuhimu wa mradi huu katika kuchangia uchumi wa jamii za Pwani na umelenga kuwawezesha wanawake na vijana waliopo katika mnyororo wa thamani wa rasilimali za bahari kupitia mradi wa bahari maisha.
"Tunaweka msukumo mpya wa kuongeza tija, kuongeza thamani ya mazao ya bahari na kulinda mazingira ya baharini kwa vizazi vijavyo".
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza kwa hatua za awali kwa kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini chagamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa mwani , wafugaji wa kaa, na jongoo bahari chini ya wataalamu kutoka chuo hicho kwa kushirikiana na UNDP Tanzania pamoja na mtaalamu kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM).
Profesa Nkonoki amesema kwamba wataalamu hao walitembelea maeneo manne ya mradi ambayo ni Tanga, Bagamoyo, Ugunja na Pemba na kukutana na wakulima na wafugaji kwa lengo la kupata taarifa muhimu.
Amesema kwamba katika ziara hiyo walibaini chagamoto kadhaa kubwa ikiwemo uwezo mdogo wa wakulima na wafugaji katika kutumia mbinu bora za kilimo na ufugaji pamoja na ukosefu wa vifaa vya kisiasa kama vile kamba, Taitai, na mashine za kusaga mwani.
"Baada ya kubaini chagamoto hizo chuo hiki kwa kushirikiana UNDP Tanzania tuliandaa programu ya mafunzo maalumu kwa wakulima wa mwani, wafugaji wa kaa, wafugaji wa jongoo bahari kutoka Ugunja, Pemba Tanga na bagamoyo"amesema
Vilevile amesema wanufaika wa mradi huo walipewa mafunzo ili kuwawezesha kuboresha uwezo wao katika maeneo muhimu kama vile kuwapatia mbinu bora za kilimo cha mwani, unenepeshaji wa kaa, ufugaji wa jongoo bahari na utunzaji wa kumbukumbu za fedha.
Suzana Mwita ambaye ni mkulima wa zao hilo kutoka Bagamoyo akiwawakilisha wakulima wenzake, ameiomba Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuwajengea kiwanda cha kuchakata mwani ili kusaidia kujiweka mguu sawa kufikia mafanikio ya uchumi wa buluu.










No comments:
Post a Comment