NA MAGENDELA HAMISI
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema vituo vya kupigia kura mkoani humo vimeongezwa kwa lengo la kutoa nafasi kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 nchini.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na Waandishi wa Habari, Chalamila amefafanua kuwa sababu ya kuongeza vituo hivyo ili kuondoa malalamiko yaliyokuwepo awali kwamba vituo vya kupigia kura havitoshi hivyo kungekuwa na uwezekano wa kuleta changamoto ya muda kwa wapiga kura na pengine visingetosha.
“Naamini sasa baada ya vituo kuongezwa hakutakuwa na malalamiko namuda utatosha kwa waliojiandikisha kuweza kupiga kura kwa haraka na kwenda kwenye majukumu mengine, hivyo nawaomba wana Dar es Salaam wajitokeze kwa wingi kuwachagua viongozi wanawataka,” amesema.
Ameongeza kuwa kinachotakiwa ni kwa wana Dar es Salaam ambao wamejiandikisha kufika mapema katika vituo vya kupigia kura ambapo saa 12 asb vituo vitafunguliwa tayari kwa mchakato huo na itakapofika saa 10 jioni wale ambao watakuwa kwenye mstari ndio watakamilisha upigaji kura.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam, amefafanua kuwa siku za kujiandikisha zilikuwa sita hadi saba ingawa siku ya kupiga kura ni moja, hivyo kila mmoja anaweza kujiuliza inawezekanaje kutumia siku moja kupiga kura na ameweka bayana kwamba ndio sababu ya kuongeza vituo vya kupiga kura kulingana na idadi ya waliojiandikisha kupiga kura.
Amefafaanua kwamba Dar es Salaam kwa mujibu ya Sensa, ina watu zaidi ya mil 5.3 na wenye miaka 18 ni laki 3 na mitaa yote inatarajiwa kuwa na wenyeviti 564, hivyo ni vema wana Dar es Salaam ambao wamejiandikisha wakajitokeza kuchagua viongozi wao.
Aidha ameongeza kuwa katika mchakato huo, wakazi wa Dar es Salaam, wasiwe na hofu ya aina yoyote kwani ulinzi umeimarishwa na yeyote atakayejaribu kuleta fujo atashughulikwa kikamilifu kupitia vyombo la dola vitakavyotawanywa Dar es Salaam nzima.
Chalamila, amesisitiza kwamba, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, wakati wote anahimiza matumizi ya 4R, hivyo matumaini kuona wanasiasa na mashabiki wa siasa hawaenda kinyume, kikubwa anawataka wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa kupiga kura kwa amini na utulivu.
Amesema kinachotakiwa ni kuionesha dunia kwamba Tanzania imekomaa kisiasa kutokana na watu wake na wanasiasa kwa ujumla kufanya uchaguzi utulivu, uhuru na amani ili wengine waendelee kujifunza kudumisha amani na utulivu kupitia watanzania, hususan katika kipindi cha uchaguzi.






No comments:
Post a Comment