BANDARI DAR YAPOKEA MELI KUBWA KUTOKA CHINA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, December 9, 2024

BANDARI DAR YAPOKEA MELI KUBWA KUTOKA CHINA

 

Meneja   wa Zimamoto na Usalama kutoka  Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  Bw. Mussa Biboze (katikati) aliyemuwakilisha  Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce  Mbossa  akiongoza kukata keki wakati  wa hafla fupi  ya kuipokea meli  kubwa ya mizigo  ya ‘EverGreen Line group’ kwenye  Bandari ya Dar es Salaam jana.

NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kupokea meli kubwa za  mizigo katika bandari yake ya Dar es Salaam, ikiwa ni  sehemu ya mafanikio baada ya uwekezaji mkubwa kufanyika katika bandari hiyo uliopeleka maboresho mbalimbali ya utendaji na utoaji huduma.


Akizungumza  na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kwenye  hafla fupi  ya kuipokea  meli kubwa  ya mizigo inayoitwa EverGreen Line Group  ikitokea nchini China yenye uwezo wa kusafirisha zaidi ya makontena elfu nne, Meneja   wa Zimamoto na Usalama wa mamlaka hiyo  TPA,  Mussa Biboze alisema  uwekezaji na uboreshwaji mkubwa uliofanywa katika bandari hiyo  umekuwa ukiwavutia  wawekezaji pamoja na mawakala mbalimbali wa makampuni za meli kuleta meli zao kupitia Bandari hiyo.


“Uwekezaji mkubwa  wa miundombinu uliofanywa na  Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika  Bandari ya  Dar es Salaam umechangia   kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kiutendaji na hivyo kuvutia kampuni kama  EverGreen Line Group kuleta meli yake kwenye bandari yetu,” alisema Biboze.


Alisema miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja uwepo wa kamera za ulinzi na usalama za kutosha katika eneo lote la bandari pamoja na kuongezeka kwa krane ambazo zinasaidia kushusha na kupakia makontena ndani ya muda mfupi sana, hivyo kufanya meli isitumie muda mrefu kukaa hapo bandarini tofauti na ilivyokuwa hapo awali.


Alisema  mara ya mwisho kampuni hiyo kuitumia bandari ya Dar es Salaam ilikuwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, lakini wamerudi tena baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na wawekezaji wakiwemo  DP World na  Adan International Ports Holding .

 

‘’Napenda kukiri kuwa makampuni haya yanayosimamia gati hizi yameongeza tija kwa Serikali pamoja na kuongeza mapato, lakini pia kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaotumia bandari ya Dar es salaam’’ alisema Biboze.


Biboze alisema ujio wa meli kama hiyo  utaongeza mapato kwa TPA na Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA), huku ukitoa fursa kwa madereva wengi zaidi ambao watahitajika  kwa ajili ya kusafirisha mizigo iliyopo ndani ya makontena hayo.


Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya EverGreen Line group Tawi la Tanzania,  Mohamed Lotfy  alisema hapo awali walikuwa wanaleta mizigo kupitia meli  ndogo, lakini hivi sasa wameamua kuja na meli kubwa na hiyo yote ni kutokana na maboresho makubwa  katika utoaji huduma yaliyofanyika katika bandari hiyo.


‘’Utafiti tulioufanya umetupa nguvu ya kuleta meli yetu  kubwa  ambayo ina uwezo wa kubeba makontena elfu nne.


Hivyo,  tutakuwa na safari moja kila mwezi na baadae tutakuwa na safari mbili kwa mwezi ili tuweze kuleta mizigo zaidi, alisema Lotfy.


Naye Meneja Kitengo cha Biashara na Mahusiano wa Tanzania East Africa Gateway Terminal Ltd Donald Talawa alisema ni mafanikio makubwa kupata meli kama hiyo yenye uwezo wa kuchukua makontena mengi zaidi kwa wakati mmoja.


‘’Sisi tuko tayari kuipokea na kuihudumia meli hii ambayo ni mpya na ya kisasa ambayo imekuja moja kwa moja kutoka nchini China,”


“Napenda nikiri kwamba maboresho yaliyofanywa hapa Bandarini yanaruhusu aina ya meli kama hizi kufika kwa sababu ya kuongezwa kwa kina cha bandari’’ alieleza Talawa.


Hafla hiyo ya upokeaji wa meli hiyo pia ilihudhuriwa na Meneja Udhibiti wa Huduma za Meli kutoka katika Shirika la uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) 

Fatma Masenene .


Fatma  alisema ujio wa meli hiyo ni neema kwa Serikali kwa sababu inapata mapato, wamiliki wa bandari kavu, na wafanyabiashara wa bidhaa ndogo ndogo kama vile wa vyakula na maji na hata watu wa usafi watafaidika pia.


No comments:

Post a Comment