NA MWANDISHI WETU
WAKATI Tanzania ikiadhimisha siku ya Maadili Duniani kesho Desemba 10, 2024, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoani Pwani, imetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.
Siku ya maadili kimataifa imeadhimishwa duniani kote leo, Desemba 9, 2024 na Tanzania inaadhimisha kesho kutokana kupisha siku ya Uhuru wa Tanganyika ambayo inaadhimisha kila mwaka ifikapo Desemba 9.
Mkuu wa Takukuru mkoani Pwani, Christopher Myava amesisitiza kwamba maadhimisho ya Maadili ambayo yanaadhimishwa kesho kitaifa, yawe chachu kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU kwa lengo la kuijenga Tanzania isiyokuwa na vitendo vya rushwa kwa maslahi ya taifa kwa ujumla.
“Ni dhahiri wananchi wakiendelea kikamilifu kutoa taarifa zinazohusu vitendo vya rushwa zitasaidia kuondosha rushwa nchini, hivyo niwasisitize wanapoona vitendo hivyo wawasiliane nasi kwa namba ya bure 113 na namba ya Mkuu wa Takukuru mkoani Pwani ambayo ni 0738 150 176,” amesema.
“Pia niwasisitize wananchi kwamba mwakani kuna Uchaguzi Mkuu, wajiandae kuwemo katika mchakato wa kuchagua viongozi wasio na makando ama wanaojihusisha na rushwa na wanatakiwa kuchagua viongozi kwa kufuata taratibu za haki na wasijiingize kwenye vitendo vya rushwa,” amesema
Ameongeza kuwa kaurimbiu ya siku ya maadhimisho ya maadili inasema “Tumia haki yako ya demokrasia kuchagua viongozi waadilifu wanaozingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa maendeleo ya taifa letu.”
No comments:
Post a Comment