NA WAF, KILIMANJARO
SERIKALI imetoa Shilingi Bilioni Nne (4) kati ya Bilioni 5.2 zinazotarajiwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa kitengo cha kisasa cha tiba ya mionzi kwa ajili ya saratani kwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC).
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, Desemba 16, 2024 kwa niaba ya Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, wakati akikabidhi magari mawili ya wagonjwa na vifaa kumi vya kufuatilia mwenendo wa wagonjwa (monitors) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC ikiwa ni hatua inayolenga kuboresha ubora wa huduma za afya hiyo.
"Serikali imejizatiti kuimarisha huduma za afya kwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa na kuongeza tija na ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wananchi,"amesema Dkt. Mollel.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya KCMC, Prof. Gileard Masenga, amesema hospitali hiyo imeendelea kunufaika na miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya huduma za afya.
"Serikali imewekeza katika ujenzi wa kitengo cha tiba ya mionzi kwa ajili ya saratani, mradi unaogharimu Shilingi Bilioni 5.2," amesema Prof. Masenga.
Naye mwakilishi wa Benki ya Maendeleo amebainisha kuwa hospitali hiyo imepokea Shilingi Milioni 60, fedha zilizokusanywa kupitia mbio za hisani ya Benki ya Maendeleo zilizofanyika jijini Dar es Salaam zikikusudiwa kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye kuboresha huduma za afya.
Dkt. Mollel akiwa hospitalini hapo ametumia ziara hiyo kuzungumza na watumishi wa Hospitali akisisitiza umuhimu wa kujituma na kutoa huduma bora kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment