MFUKO WA VIJANA UTAWAWEZESHA WABUNIFU - WAZIRI KIKWETE - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, December 20, 2024

MFUKO WA VIJANA UTAWAWEZESHA WABUNIFU - WAZIRI KIKWETE


NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema itahakikisha inafungua milango ya mitaji kwa wabunifu, ili waweze kuchangia ukuwaji wa uchumi na huduma za kijamii.


Hakikisho hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete wakati akifunga Tamasha la Tanzania Startups Association (TSA), lililofanyika kwa siku tano katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).


Kikwete amesema serikali inaunga mkono juhudi za TSA katika kuendeleza wabunifu, hivyo yeye kama waziri kijana atahakikisha wanatumia fursa zilizopo kwa kuhakikisha wanapata mitaji ili kuendeleza bunifu zao.


"Serikali ina jukumu la kusaidia juhudi za vijana wabunifu ili kukuza vipaji na mitaji, hivyo mimi sijisikii vizuri kuona wabunifu wanakosa mitaji, hivyo nitatumia nafasi yangu kuhakikisha vijana wanapata taarifa za fursa zilizopo serikalini, ikiwemo mfuko wa vijana ambao unalenga kusaidia bunifu kama hizo ambazo zinabuniwa," amessma.


Waziri Kikwete amesema serikali itatumia rasilimali zake na kushirikisha wadau wa sekta mbalimbali kuhakikisha wanatoa fedha kwa ajili ya wabunifu ambao wanakuja na bunifu zenye kuchochea ukuaji wa uchumi na jamii.


Amesema Agosti 2024 wizara imezindua Sera ya Vijana, ambayo inataka Startups ziwezeshwe, hivyo wamejipanga kutoa elimu kwa wadau wote kuhusu sera hiyo na kuangalia namna ambavyo wanaweza kutekeleza wanachotaka wabunifu.


Amesema kupitia sera hiyo wabunifu watapata fursa ya kuanisha changamoto zao.


"Dhamira ya serikali kusaidia kundi la vijana ipo ndio maana katika mwaka huu wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 16 ambapo kwa wahitaji wangepewa iwapo wameomba," amesema.


Waziri Kikwete amesema serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwakomboa wananchi kiuchumi na kijamii, hivyo kuwataka wabunifu wasisite kutumia fursa zilizopo.


Amesema wizara yake inaunga mkono bunifu zote zinazofanywa na watanzania na kuahidi kutoa msukumo kwa kila mdau kushiriki.


Kikwete amesema pia watahakikisha wabunifu wanakuwa na mazingira rafiki ambayo yatawapa moyo wabunifu ili wawe na bunifu nyingi kwani ushahidi unaonesha kuwa zinalipa.


Waziri Kikwete amesema Startups ni sehemu ya biashara zinazolenga kukua kwa haraka zaidi kwa kutumia bunifu mpya na za kiteknolojia kwa kuleta suluhisho jipya na kwa haraka zaidi.  


Mkurugenzi Mkuu wa Startups Association Zahoro Muhaji amesema kuwa tamasha hilo limekua na mafanikio  makubwa na kwamba  Startups imekua ikichangia pato na ajira kwa vijana wengi.


"Ndani ya miaka minne iliyopita Startups imevutia Tanzania uwekezaji wa dola za Marekani milioni 300, lakini kwa mujibu wa Tume ya Taifa Sayansi na Teknologia (COSTECH), ajira kupitia eneo hilo ni zaidi ya laki moja, tunaona kwa siku zijazo sekta hii ya ubunifu itakuwa na mchango mkubwa zaidi," amesema.


Muhaji amesema Startups imeweza kushika uchumi wa dunia kwani kwa sasa kati ya kampuni 10 tajiri kampuni saba yanatoka kwenye teknolojia na uchumi wa kidigitali.


Mkurugenzi huyo amebainisha changamoto wanayokabiliana nayo ni kukosekana kwa sera ya Startups na kwamba ikiwepo itaweza kuikuza sekta hiyo kimitaji, kikodi na usajili.


Aidha, Muhaji alipongeza kwa serikali kutoa zaidi ya sh bilioni 2.5 ambazo zinasimamiwa na COSTECH kwa ajili ya kuwezesha vijana wabunifu.


Mkurugenzi huyo amesema pia wanaomba serikali kuwasidia kupata ofisi ya kudumu ambayo itaweza kuwapunguzia gharama.


Muhaji amewataka wabunifu kuja na bunifu nzuri na kulipa soko fursa ya kuamua.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Smart Pika, Andron Mendes ambaye ubunifu umeweza kubadilisha maisha yake na kuwa bilionea, amesema amefikia hapo kutokana na kutokata tamaa na kusimamia dhamira yake.


"Mimi wakati nikiwa mwaka wa tatu UDSM niliona kuna fursa ambayo haijatumika hivyo nimepambana bila kukata tamaa miaka minne na kusema kweli imenilipa," amesema.


Mendes amewataka vijana wasikate tamaa katika kile ambacho wanaamini, ili waweze kufikia ndoto zao.


Mkurugenzi huyo amesema kupitia bunifu zake kuanzia mwakani ataanzisha kampuni zingine mbili ambazo zitamuwezesha kutoa ajira zaidi 400.


Naye Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CODE255 Development Technologies, Mhandisi Noel Lema ameiomba serikali kuweka mazingira rafiki na kuwapatia mitaji wabunifu ili waweze kuendeleza bunifu zao.


Lema amesema vijana wa kitanzania wabunifu nyingi lakini wanashindwa kuziendeleza kutoka na ukosefu wa mitaji.


"Sisi tumebuni teknolojia nyingi kwenye mafuta, umeme, maji na nyingine, hivyo tukiwezeshwa tutaweza kuchangia pato la taifa na kutoa ajira nyingi," amesema.







No comments:

Post a Comment