NA MWANDISHI WETU
OFISI ya Waziri Mkuu, kupitia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa kimbunga “CHIDO” katika Bahari ya Hindi.
Mwenendo wa Kimbunga “CHIDO” kwa siku ya jana Alhamisi tarehe 12 na leo Ijumaa
Disemba 13, 2024, kimeendelea kusalia katika eneo la bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar huku kikiendelea kuashiria kuelekea katika maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji katika kipindi cha siku tatu zijazo (tarehe 14 hadi 16 ya mwezi Disemba, 2024).
Aidha, kimbunga hicho bado hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja hapa nchini.
Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga “CHIDO” kinatarajiwa kupita (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya mkoa wa Mtwara na maeneo jirani hususan kwa siku ya tarehe 15 Disemba 2024.
Vilevile, upo uwezekano wa kutokea matukio ya upepo mkali wa bahari unaofika kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofika mita 2 katika maeneo ya mwambao wote wa pwani ya nchi yetu hasa kwa siku ya tarehe 15 Disemba, 2024.
USHAURI: Watumiaji wa bahari, wananchi wanaoishi kando kando ya bahari na waliopo
katika mikoa ya kusini wanashauriwa kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Vilevile, Mamlaka za Serikali za Mitaa zikiongozwa na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za mikoa,
wilaya, kata na kijiji/mtaa zinatakiwa kuendelea kuchukua hatua za tahadhari na kusimamia utekelezaji wake kwa wananchi waliopo katika maeneo yao.
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa kimbunga hicho na kutoa taarifa kwa umma kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki.
No comments:
Post a Comment