NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
WAKURUGENZI wa Kampuni za Mikopo ya Kidigitali ya Kisasi Finance na Awallet Afrika Limited ambazo zinaendesha taasisi za mikopo za Loan Plus, Swift Loan wamepewa siku 14 kulipa fidia ya shilingi 100 milioni kwa vitendo vya udhalilishaji kwenye mitandao na kusambaza taarifa za uongo.
Taasisi hizi, licha ya kuwa ni kati ya taasisi 69 ambazo benki kuu (BOT), Novemba 21,2024 ilitangaza kuzifungia kutokana na kufanyakazi bila ya kuwa na kibali na kushindwa kufanyakazi kwa kuzingatia sheria za uwazi, uwekaji wa tozo na riba, njia ya ukusanyaji madeni, utunzaji taarifa binafsi za wateja na kulinda faragha, zimekuwa zikiendelea na kazi.
Akizungumza na waandishi wa Habari Wakili John Shirima wa Kampuni ya J&J Shirima Associates&Co kwa niaba ya jopo na Mawakili 10 ambao wamejitokeza kumtetea mlalamikaji, Mussa Juma, alisema wamewapa notisi ya siku 14 kuanzia Desemba 13,2024, wakurugenzi wa Kisasi Finance na Awallet Afrika Limited kulipa fidia ya Sh milioni 100 na kumuomba radhi kwa maandishi .
Shirima alisema Katika notisi hiyo, ambayo nakala imepelekwa BOT na polisi ambapo pia kesi ya jinai ARS/RB/12589/2024 imefunguliwa ya kusambaza lugha ya matusi mtandao, wakurugenzi hao kupitia wafanyakazi wake, wanatuhumiwa kuwa walisambaza taarifa kwenye mitandao yenye matusi ya nguoni na udhalilishaji na taarifa za uongo kuwa Mama mzazi wa Mussa Juma amefariki na kuanza kuomba michango.
Alisema wafanyakazi wa kampuni hizo, wamekuwa wakitumia namba za 0774652645, 0755365471, 0617512622, kusambaza matusi mitandaoni kulazimisha kupewa fedha la sivyo, wataendelea kusambaza tarifa za uongo mitandaoni licha yakupewa maelezo hakuna deni ambalo linadaiwa.
Hata hivyo, alisema Desemba 12 baada ya Meneja wa Taasisi ya Loan Plus namba 0713694907 kupata taarifa ya shauri hili kufikishwa polisi, ilisambaza taarifa kwenye simu za watu mbali mbali, ikiomba radhi ya kutoa taarifa za uongo juu ya Mussa kuwa anadaiwa na kampuni hiyo .
Wakili Hamis Mayomba ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) Kanda ya Arusha alisema kampuni hizo zinachofanya ni makosa kwanza kosa la matumizi mabaya ya mtandao, sheria ya ulinzi wa faragha na sheria za BOT.
Mmoja wawafanyakazi wa taasisi ya Loan Plus, Jamira Chakachaka baada ya kutakiwa kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma hizo, alisema wataendelea na kazi yao na wasipopewa fedha wataendelea kusambaza taarifa za kashfa.
“Nendeni popote”mnajisumbua tu usifikiri hizi ni kampuni ndogo tupo na hao hao viongozi wa Serikali na hata hao BOT wala hatuwaogopi ndio sababu walitangaza tusifanyekazi tunaendelea na kazi na hata TCRA hawawezi kutufanyakitu ndio sababu hadi sasa tupo hewani” alitamba.
Kamanda polisi mkoa Arusha, Justine Masejo alieleza kupata taarifa za kufunguliwa shauri hilo na udhalilishaji na tayari maafisa wa polisi kutoka Arusha wameanza uchunguzi wa tukio hilo, ikiwepo kutumwa maafisa jijini Dar es Salam kuwasaka wahusika.
Kwa muda mrefu kampuni za mikopo mitandaoni, zimekuwa zikilalamikiwa na mamia ya wananchi kwa ukiukwaji wa sheria, utapeli na kudhalilisha watu mitandao na tayari Bunge la Jamuhuri ya Muungano lilitaka Serikali kuchukuwa hatua.
Hivi karibuni, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Gavana wa Benki kuu, Emmanuel Tutuba walitoa tamko juu ya taasisi hizo za mikopo mitandaoni kukiuka sheria na baadhi kufungiwa.
Hata hivyo, licha BOT kusitisha utendaji wa kazi kwa taasisi hizo zimeendelea na kazi na licha ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kutakiwa kuzifunga kampuni hizo kutumia mitandao lakini bado zipo hewani.
No comments:
Post a Comment