NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameahidi kuwapa ushirikiano wakuu wa taasisi hizo na kuendeleza yale yote ambayo yapo katika utekelezaji ili kuchochea maendeleo.
Ulega amesema hayo baada ya kukukutana na kufanya mazungumzo na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi katika Ofisi ndogo za Wakala ya Barabara (TANROADS), leo tarehe 11 Disemba, 2024 Dar es Salaam.
Amesema wizara hiyo ina majukumu mengi ya kuchochea maendeleo na msingi wa kufika huko ni ushirikiano
"Majukumu makuu ya Wizara ni ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, vivuko, majengo na nyumba za watumishi na viongozi wa Serikali, hivyo tunapaswa kushirikiana kuhakikisha kufikia malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan na serikali kwa ujumla," amesema.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, pamoja na Wakuu wa Taasisi kutoka TANROADS, Wakala wa Majengo (TBA), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili ya Wakandarasi (CRB), Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) na Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT).
Waziri Ulega amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumuamini na kumteua kuhudumu katika Wizara ya Ujenzi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Aisha amemkaribisha Waziri Ulega na kumuahidi ushirikiano kutoka kwa Menejimenti na watumishi wa Wizara pamoja na Taasisi zake.
No comments:
Post a Comment