MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola katika operesheni zilizofanyika mwishoni mwa mwaka 2024 zilikamatwa kilogramu 673.2 za methamphetamine na heroin.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo ameyasema hayo, Januari 9,2025 wakati akitoa taarifa za dawa za kulevya nchini mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa,mafanikio hayo yamechagizwa na juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kupambana na kudhibiti dawa za kulevya nchini kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa ujumla.


Pia, Kamishna Jenerali Lyimo amesema,pamoja na ukamataji wa dawa hizo, DCEA ilijikita katika kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya na kuimarisha huduma za matibabu ya waraibu.

Amesema,kati ya dawa hizo kilogramu 448.3 zilizowahusisha raia nane wa Pakistani zilikamatwa Bahari ya Hindi zikiwa zimefichwa ndani ya jahazi lililosajiliwa nchini Pakistani kwa namba B.F.D 16548.

Vilevile Kamishna Jenerali Lyimo amesema, kilogramu 224.9 zilikamatwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam.


“Kwa mwaka 2024, jumla ya kilogramu 2,327,983.66 za dawa za kulevya zilikamatwa, ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini.

“Mafanikio haya yamewezekana kwa ushirikiano wa vyombo vyote vya ulinzi, wadau wa ndani na nje ya nchi na wananchi kwa ujumla.”