RITA YATOA MAAGIZO MAZITO KWA TAASISI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, January 7, 2025

RITA YATOA MAAGIZO MAZITO KWA TAASISI


Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Frank Kanyusi, akizungumza na wadau mbalimbali na Mamlaka za juu za Bodi za Wadhamini (hawapo pichani) kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, wakati wa kikao kilichofanyika mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki.


NA MWANDISHI WETU, MOROGORO 


WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) imeziagiza Bodi za Wadhamini wa Taasisi kuhakikisha zinatimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwakilisha marejesho ya kila Mwaka (annual returns)


Akizungumza wakati wa kikao na wadau mbalimbali na Mamlaka za juu za Bodi hizo kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, hivi karibuni mkoani Morogoro, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi alisema kikao hiko kililenga kubadilishana uzoefu kuhusu kuimarisha usimamizi na udhibiti wa Bodi hizo kwa maslahi mapana ya wanachama wa taasisi zao sambamba na taifa kiujumla.


 "Nitumie nafasi hii kuzitaka taasisi  mbalimbali kufika RITA na kusajili Bodi za Wadhamini kwani hivi karibuni kikosi kazi kitapita na kufanya ukaguzi na Taasisi zitakazo bainika kuendesha shughuli zao bila ya usajili zitachukuliwa hatua stahili za kisheria," alisisitiza. Kanyusi.


Kanyusi alibainisha kuwa Bodi za Wadhamini zinapaswa kwa mujibu wa Sheria kutekeleza majukumu yao ya msingi kwa maslahi ya Taasisi wanazozisimamia na hawatakiwi kuwa na manufaa au faida binafsi na vile vile wanapaswa kujua rasilimali na madeni ya Taasisi husika.


"Kwa mujibu wa sheria ya Muunganisho wa Wadhamini Sura ya 318, Taasisi zinazotakiwa kuwa na Bodi ya Wadhamini ni pamoja na vyama vya siasa, taasisi na madhehebu ya kidini, vyama / vilabu vya michezo mfano: mpira wa miguu, mpira wa mikono, mpira wa vikapu nk, Taasisi binafsi za kijamii zinazomiliki mali, vyama vya Kiuchumi na vyama vya kitaaluma, "


Nakuongeza kuwa "Sheria hiyo inampa Mamlaka Kabidhi Wasii Mkuu kuwa ndio Mdhamini Mkuu mwenye jukumu la kusimamia na kuratibu Usajili na kudhibiti utendaji wa Bodi za Wadhamini," alisema Kanyusi.


Kanyuzi alisema  pamoja na sheria kuainisha majukumu na wajibu wa Bodi za Wadhamini, bado kuna changamoto kwa baadhi ya taasisi hasa za kidini, vilabu vya michezo na vyama vya siasa kwa Wadhamini kutokuwa waadilifu na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. 


Natumani tukishirikiana kwa pamoja na wadau wetu na kila mmoja akitimiza wajibu wake kikamilifu katika eneo lake basi tutaweza kuokoa fedha na mali zinazofujwa, kupotea au kutumika kinyume cha malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hizo alisema Kanyusi.


Kwa upande wake Msajili wa Jumuiya za kiraia kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani Emmanuel Kihampa alisema kuwa  Jumuiya zinazosajiliwa zinapata uhalali wa kisheria lakini ili ziweze kutekeleza majukumu yao lazima ziwe na utu wa kisheria baada ya kusajili Bodi za Wadhamini RITA.


 Kuna changamoto kubwa ya migogoro katika taasisi za kidini na vyama vya siasa      inayochangiwa na kugombania mali zilizopo kwenye taasisi hizo ambazo hazina Bodi za wadhamini ambao walitakiwa kuwa ndiyo wasimamizi na waangalizi wa mali hizo," alisema   Kihampa.


Naye mwakilishi wa Msajili wa Vyama vya siasa ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria Muhidini Mapeyo alisema kwa upande wao wameshafanya marekebisho ya sheria sura ya 258 ili kutenganisha majukumu ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa na Bodi za Wadhamini kwa lengo la kuzuia mgongano wa kimaslahi na kuwezesha kutoingiliana kwenye majukumu na usimamizi wa mali za vyama hivyo.


Kupitia sheria hii iliwaondosha viongozi wakuu kuwa Wadhamini katika Bodi za vyama vyao tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walijipenyeza na kushika nyadhifa zote mbili kwa pamoja, jambo ambalo lilichangia ufujaji wa mali za vyama na matumizi mabaya ya madaraka," alisema Mapeyo.


 Kikao hiko kimewakutanisha Wadau mbalimbali kutoka Msajili wa Vyama vya Kijamii, Benki Kuu ya Tanzania, ofisi ya Kamishna wa Ardhi, ofisi za Makatibu Tawala wa wilaya za mikoa, ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, Umoja wa Mabank Tanzania (Tanzania Bankers Association), Mamlaka za uongozi za kidini BAKWATA, TEC, CCT, SDA, FPCT na Baraza la Michezo Tanzania (BMT)

Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Frank Kanyusi, ( katikati)  akiwa kwenye picha ya pamoja na  wadau mbalimbali na Mamlaka za juu za Bodi za Wadhamini kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, wakati wa kikao kilichofanyika mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki.

No comments:

Post a Comment