NA MWANDISHI WETU
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu, amesema kuwa umeme ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo Wizara ya Nishati itahakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme ya uhakika.
Dkt. Kazungu Ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu Mkoani Morogoro, kinachozalisha megawati 204.
Ameongeza kuwa, ni muhimu kusimamia miradi ya uzalishaji umeme ili kuwa na usambazaji wa nishati kwa ufanisi na kuhakikisha kwamba maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanapata nishati hiyo.
"Wizara ya Nishati ina jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme ya uhakika kwa ajili ya kusukuma mbele shughuli mbalimbali za maendeleo." Amssema Dkt. Kazungu
Katika ziara hiyo, amebainisha kuwa kituo cha Kidatu kilianza kuzalisha umeme tangu mwaka 1975 na kwa sasa kinatimiza miaka 50 ya huduma hivyo ameielekeza TANESCO kufanya upembuzi yakinifu na ukarabati wa kituo hicho ili kiendelee kuzalisha umeme kwa ufanisi.
Akiwa kwenye kituo hicho, Dkt. Kazungu amekagua mtambo namba mbili unaofanyiwa ukarabati ulioanza mwezi Mei mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika Januari 2025 na kutoa maagizo kwa TANESCO ya kuhakikisha kuwa mkandarasi anasimamiwa kwa karibu ili kazi hiyo iweze kukamilika kwa wakati na mtambo huo uweze kuungana na mitambo mingine ambayo itaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme.
Meneja wa Mradi katika kituo hicho cha Kidatu Mhandis Manfred Lucas amesema TANESCO itaendelea kuhakikisha kituo cha kufua umeme cha kidatu mitambo yake inakuwa katika hali nzuri na inafanya kazi muda wote ili kuchangia umeme wa kutosha kwenye gridi ya Taifa na kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment