NA MWANDISHI, KIBAHA
MADIWANI wanne wa Viti Maalum waliomaliza muda wao kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini wamefanikiwa kushinda kwenye uchaguzi wa kura za maoni kupitia chama hicho.
Aidha Madiwani hao wanne walikuwepo kwenye Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha lililopita wanaungana na diwani mmoja ambaye ameingia kwenye nafasi hiyo kwa mara ya kwanza.
Kwenye uchaguzi wa Madiwani huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Nexus Kibaha Madiwani hao walioshinda ni kati ya watia nia 15 waliojitokeza kuwania nafasi tano zilizokuwa zikigombaniwa za Tarafa mbili za Kibaha na Kongowe.
Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo Ally Kibwana ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mafia alimtangaza Diwani Aziza Mruma kutoka Tarafa ya Kibaha kuwa ndiye aliyeibuka mshindi kwa kupata jumla ya kura 952 kati ya kura halali 1,083 zilizopigwa.
Mshindi wa pili alikuwa Sara Uledi ambaye ameingia kwa mara ya kwanza alipata kura 864 kutoka Tarafa ya Kongowe akifuatiwa na Shufaa Mshana kutoka Tarafa ya Kibaha aliyepata kura 581 na Lydia Mgaya kutoka Tarafa ya Kongowe aliyepata kura 575 na Selina Msenga kutoka Tarafa ya Kibaha aliyepata kura 527.
Kwa matokeo hayo Aziza Mruma, Shufaa Mshana na Selina Msenga kutoka Tarafa ya Kibaha wamefanikiwa kuwa washindi huku Sara Uledi na Lydia Mgaya kutoka Tarafa ya Kongowe wameshinda.
Kibwana aliwataja wagombea wengine na kura walizopata Tarafa ya Kibaha iliyokuwa na wagombea 9 ni Meri Msimbe kura 420, Emiliana Sinesilya 294, Beatrice Manyama 192, Rehema Abdala 103, Joyce Shauri 74 na Magreth Yagaza.
Aliwataja wagombea kutoka Tarafa ya Kongowe kuwa ni Tatu Mshindo kura 343, Mariam Gama 180, Elizabeth Nyambilila 113, na Beatrice Kesi 99 jumla ya kura 1,094 zilizopaswa kupigwa kura halali zilikuwa 1,083 na kura 11 ziliharibika.
No comments:
Post a Comment