NA MWANDISHI WETU, SAME
MKUU wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amewaasa askari wa Jeshi la Akiba (Mgambo) kutanguliza mbele Uzalendo, kuwa walinzi wa kweli wa amani pamoja na mshikamano wa kijamii katika maeneo yao wanayoishi.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya kulenga shabaha yaliyofanyika katika Kata ya Bangalala, Wilaya ya Same, Kasilda alisema kuwa ni jukumu la askari wa Jeshi la Akiba mojawapo ni kuwa walinzi wa kwanza wa amani katika maeneo yao.
“Mtakapofika uraiani ni lazima mjitofautishe, wananchi wakikuoneni waone wako mikononi salama chini yenu, ninyi ni walinzi wa amani. Msiwe watu wa kuanzisha vurugu, bali muishi kama askari wazalendo,” alisema Kasilda.
Aidha, aliwasisitiza kuhakikisha wanakuwa na matumizi sahihi ya silaha, kuepuka visasi na kuwasaidia wananchi kwa kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kuwa raia wema.
Mkuu huyo wa wilaya pia alikemea vitendo vya rushwa, akiwataka askari hao kulinda amani na mshikamano wa kijamii hasa katika kipindi hiki kinapoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, utakaofanyika Oktoba 29.
Jeshi la Akiba lipo kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Akiba. likiwa na jukumu la kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda amani na usalama wa nchi.
No comments:
Post a Comment