Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo siku ya Jumamosi, Agosti 30, 2025.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya CCM Kisiwandui, Mkoa wa Mjini Magharibi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Komredi Khamis Mbeto, amesema Dk. Mwinyi atachukua fomu katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufuatia taratibu na mwongozo uliowekwa na Tume hiyo.
Amesema kuwa kwa mujibu wa ZEC, wagombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, Uwakilishi na Udiwani wanatakiwa kuchukua fomu kuanzia Agosti 28 hadi Septemba 10, 2025, ambapo uteuzi wa wagombea utafanyika Septemba 11, 2025 na kufuatiwa na kuanza rasmi kwa kampeni.
Aidha, Mbeto ameeleza kuwa safari ya kuchukua fomu ya Dk. Mwinyi itaanzia nyumbani kwake Migombani, kisha kuelekea Ofisi za ZEC akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa CCM. Baada ya kukamilisha taratibu hizo, atarejea Makao Makuu ya Chama kupitia gari la wazi, na hatimaye kuelekea katika Kiwanja cha Mau kwa ajili ya kuzungumza na wananchi.
No comments:
Post a Comment