TAASISI YA UTAFITI, TAIWAN KUSHIRIKIANA KUKUZA KILIMO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, August 6, 2025

TAASISI YA UTAFITI, TAIWAN KUSHIRIKIANA KUKUZA KILIMO


 NA MWANDISHI WETU, ARUSHA


TANZANIA inategemewa kuzalisha wataalamu wa uzalishaji wa mbegu bora chotara za mazao mbalimbali baada ya Chuo Kikuu cha Taiwan kuonesha utayari wa kuanzisha programu za mafunzo katika Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendeshaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika ‘World Vegetable Centre’ kilichopo Tengeru mkoani Arusha.


 


Akiongea wakati wa mafunzo yanayohusu uzalishaji mbegu bora ya mazao mbalimbali yanayohimili magonjwa na ukame, Dk. Sognigbe N’Danikou, mtaalamu wa uzalishaji mbogamboga asili na utunzaji kutoka katika taasisi hiyo jijini hapa, amesema kuwa ushirikiano na chuo hicho unalenga  kukuza kilimo hapa nchini kupitia maeneo mbalimbali.


 


 


Amesema miongoni mwa maeneo hayo ni kufanya tafiti mbalimbali kuhusiana na uzalishaji na utunzaji wa mbegu ‘chotara’ zenye kukua kwa haraka na kuhimili magonjwa na ukame.


 


Amesema kupitia mpango wa Taiwan wa kukuza Kilimo cha Mbogamboga barani Afrika ( Taiwan-African Vegetable Initative (TAVI), kituo hicho kitashirikiana na taasisi nyingine hapa nchini ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ili kukuza sekta ya kilimo, kuzalisha wataalam wa kutosha na kuwafikia wakulima wengi zaidi.  


 


Amesema maeneo mengine ambayo Tanzania itafaidika kupitia ushirikiano huo ni pamoja na uzalishaji wa wataalamu wa kutosha, kuongeza uwezo wa kufanya utafiti na ubadilishanaji wa programu za mafunzo (scholarships) juu ya uzalishaji chakula bora na lishe. 


 


Naye Profesa Chau-Ti Ting kutoka Chuo Kikuu cha Taiwan amesema kuwa Tanzania itakuwa kitovu cha uzalishaji mbegu bora na uhifadhi kupitia ushirikiano huo wenye lengo la kukuza sekta ya kilimo hapa nchini.


 


“Pamoja na maeneo mengine ya ushirikiano huu, tunategemea chuo chetu kikuu cha Taiwan kuanzisha kozi maalum katika taasisi hii ya kimataifa hapa Arusha,” amesema Profesa Ting.


 


Naye Profesa Hung –Vi Wang amesema ushirikiano huu una lengo la kuangalia njia bora za uzalishaji wa mbegu bora kupitia tafiti mbalimbali na kuangalia namna wanavyoweza kuanzisha program za mafunzo katika taasisi hiyo mkoani Arusha.


 


Mmoja wa wanaohudhuria mafunzo hayo, Daktari Aloyce Kundy kutoka Benki ya Vinasaba vya Mimea iliyo chini ya Mamlaka ya Viuatilifu na Mimea (TPHPA) amesema Tanzania imekua na mahusiano mazuri na Taiwan katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo kwa kufanya tafiti zenye kukuza sekta hiyo hapa nchini.


 


Naye Magdalena Kiungo, mwanafunzi wa Chuo cha Taasisi ya Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela anayesomea uzalishaji wa mbegu bora za kisasa amesema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya kilimo, hasa katika uzalishaji wa mbegu bora zenye kutoa mazao mengi na kuhimili ukame.


 


“Nimefurahi kuwa mmoja wa washiriki wa mafunzo haya na ushirikiano huu utakuwa na tija na kutuwezesha sisi maofisa wa kilimo wa miaka ijayo kuwa na utaalamu wa kimataifa,” amesema Bi. Magdalena.







No comments:

Post a Comment