WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa na viongozi wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) wamekutana na kujadili namna ya kutatua changamoto za wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini.
Kikao hicho kimefanyika jana Alhamisi Agosti 21 mwaka huu jijini Dodoma katika Ofisi ya Waziri Kikwete ambapo mjadala mkubwa ulijikita kwenye masuala ya mikataba ya kazi na hali bora za kufanya kazi.
Akizungumza katika kikao hicho,Waziri Kikwete, amesema wizara yake hairidhishwi na hali za wafanyakazi walio wengi katika vyombo vya habari na lazima jambo hilo lipatiwe ufumbuzi kwa kuhakikisha wanapewa mikataba kama sheria inavyotaka.
"Nimewaita hapa leo tuzungumze pamoja kuhusu changamoto za kazi katika sekta yenu, kwa kweli mimi binafsi nazijua changamoto zenu na tunataka kuzifanyia kazi, naamini kupitia kikao hiki ambacho kamishna wa kazi ameshiriki tunaweza kupata muafaka kwa siku zijazo," amesema.
Amesema anajua wanahabari wengi hawana mikataba ya kazi na ajira na wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo lazima zifike mwisho kwani sheria ya kazi ni moja kwa wafanyakazi wote, lazima ionekane kwenye sekta zote.
"Kama tulivyozungumza Arusha, tulikubaliana leo kukutana tena hapa na Kamishna wa Kazi akiwepo ili kuona ni jinsi gani tunaweza kusaidia wanahabari nchini kufanya kazi katika mazingira bora, naomba kila mtu aende kutekeleza yale ambayo yanamuhusu tuangalie njia ya kupitia yenye maslahi kwa wote," amesema
Amesema ni lazima kila sekta nchini ifanyekazi kwa kuzingatia sheria za kazi zilizopo badala ya kufanyakazi kiujanja ujanja na mwisho uzeeni kuja kutaabika ama unapopata matatizo kushindwa kujisaidia.
Kwa upande wake Kamishna wa Kazi, Mkangwa amesema Ofisi yake ipo tayari kufanyakazi na JOWUTA kusaidia kutatua changamoto za wafanyakazi katika vyombo vya habari ambapo alisisitiza kushirikiana katika kutoa taarifa za changamoto zilizopo.
Mkangwa ametumia kikao hicho kuwaasa waandishi wa habari kuhakikisha wanafanya kazi baada ya kusaini mikataba ya kazi inayotambulika kisheria .
"Tunaweza kufanya ukaguzi lakini sekta yenu ina changamoto kadhaa za kimfumo ikiwepo uwepo wa wafanyakazi wanaoandika habari kwa malipo baada ya habari kutumika (correspondent na freelance) wanahabari wenye mikataba ya muda (retainer), huu utaratibu ni mgumu sana na upo kwenu zaidi, unapaswa kuondoka ili tuwe kwenye njia moja kama sekta zingine," amesema.
Amesema ofisi yake imekuwa ikifanya ukaguzi mara kwa mara na kukuta mikataba ya walio katika ajira pekee hivyo ni vigumu kujua makundi mengine kama huna taarifa za kutosha na kutumia fursa hiyo kuomba waandishi watoe ushirikiano ili kubaini mapungufu yaliyopo.
"JOWUTA nawaomba tushirikiane ili kupata taarifa sahihi za hali za wafanyakazi katika kila chombo cha habari ili tuzifanyiekazi, " amesema
Amesema Ofisi yake pia itaendelea kutoa elimu ya sheria za kazi kwa wanahabari na wafanyakazi wengine ili wafanye kazi kwa kuzingatia sheria.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma aliomba Wizara hiyo kusaidia wanahabari kufanyakazi katika mazingira bora na sheria za kazi kufuatwa kama ilivyo katika sekta nyingine.
Amesema zaidi ya asilimia 80 ya wanahabari nchini wanafanyakazi bila kuwa na mikataba ya kisheria, bima ya afya wala mifuko ya pensheni na zaidi ya miaka 10 katika hali hiyo jambo ambalo halikubaliki.
"Tunakuomba sana Kamishna usaidie sekta hii, ili waajiri wazingatie sheria za kazi na tunaomba pia ukaguzi wa mara kwa mara katika vyombo vya habari, kuhakikisha wamiliki wa vyombo vya habari wanafuata sheria za kazi," amasema.
Awali Katibu Mkuu wa JOWUTA, Seleman Msuya amesema JOWUTA inashukuru serikali kwa kazi nzuri ambayo inafanywa na Bodi ya Ithibati Tanzania (JAB) kwa kuhakikisha wanaofanyakazi katika vyombo vya habari ni wale wenye sifa za kitaaluma.
Hata hivyo alisema ni muhimu mkazo wa kuwa na Ithibati kwa wanahabari uendane na kuboresha maslahi kwa wanahabari ikiwepo kupewa mikataba, kulipiwa bima na kuwa na stahili nyingine.
"Kwa sasa kila kukicha kuna michango ya wanahabari wagonjwa kwani wengi hawana bima wala hawapo kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Tunaomba nguvu hii ambayo imeoneshwa na JAB kwenye sifa za wanahabari ionekane kwa Kamishna wa Kazi kwenye eneo la mikataba," amesema.
Amesema waandishi wa habari ni nguzo muhimu katika huduma za kijamii, kiuchumi na kisiasa, hivyo ni vema wakapewa kipaumbele kama makundi mengine kwenye ajira.
"Tunaposema sekta inachangia kwenye pato la taifa, ni vema ikaonekana kivitendo, kwenye sekta hii ya habari yenye zaidi ya watu 30,000 mchango wake kwenye uchumi wa nchi bado ni mdogo sisi tunaamini iwapo sheria zitafuatwa mchango wetu utaonekana kila mwaka kama zilivyo sekta za utalii, uvuvi, ujenzi, kilimo na nyinginezo," amesema.
Mweka hazina wa JOWUTA Lucy Ngowi amesema sekta ya habari inapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma ili kuhakikisha waandishi wananufaika na nchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment