DOYO: SERIKALI YANGU ITAWALIPA FIDIA WAATHIRIKA WA TEMBO KITETO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, September 14, 2025

DOYO: SERIKALI YANGU ITAWALIPA FIDIA WAATHIRIKA WA TEMBO KITETO


NA MWANDISHI WETU, KITETO MANYARA

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ameendelea na ziara yake ya kampeni katika vijiji vya Kijungu na Pori kwa Pori, vilivyopo katika Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara.


Akiwahutubia wananchi wa maeneo hayo, Doyo aliwahakikishia kuwa, endapo atachaguliwa, serikali yake itajenga hospitali ya kisasa katika eneo hilo ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma bora za afya, ambayo imekuwa kero kwa muda mrefu.


Kwa mujibu wa wakazi wa Kijungu, kwa sasa hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, aidha kuelekea Kiteto Mjini au Songe katika Wilaya ya Kilindi, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao, hasa katika hali za dharura.


 “Nafahamu mnakabiliwa na changamoto nyingi, lakini changamoto ya afya inabeba msingi muhimu katika ujenzi wa taifa,” alisema Doyo. 


“Ili tujenge taifa imara, tunahitaji wananchi wenye uhakika wa huduma za afya. Kuna haja ya kujenga hospitali hapa ili msilazimike kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu,” aliongeza.



Akiwa katika mkutano mwingine na wananchi wa Kiteto Mjini, Doyo alizungumzia changamoto ya migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, akisema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakitoa taarifa zisizo sahihi huku wakiwazusishia viongozi tuhuma ambazo si sahihi na hazina msingi.


“Wakati mwingine wananchi wanakuwa waongo wanapotoa taarifa na kuwatuhumu viongozi, jambo ambalo si sahihi. 

Nikiwa Rais, nitatoa maagizo ya kuhamisha staafu yote iliyopo sasa na kuleta mpya Kiteto ili tuone mambo yanavyokwenda, na kuhakikisha tunapata ukweli na usahihi wa taarifa zenu,” alisema Doyo.


Aidha, aliahidi kuweka askari wa wanyamapori katika maeneo ya makazi ya watu ili kudhibiti tembo wanaovamia mashamba na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi.


Doyo ameahidi kuunda tume maalum itakayotengeneza ramani ya maeneo ya wakulima na wafugaji kwa kuweka mipaka ya haki kwa pande zote.

 Alisisitiza kuwa ulinzi shirikishi utaimarishwa ili kuzuia migogoro ya mara kwa mara, na akaonya kuwa serikali yake haitavumilia kundi lolote litakalokiuka makubaliano ya vikao vya kimila au serikali.


Kwa upande mwingine, aliwahakikishia wananchi wote walioathiriwa na uvamizi wa tembo kuwa watapatiwa fidia stahiki kama kifuta jasho kutokana na madhara hayo.



Msafara wa kampeni wa mgombea huyo unaendelea na ziara zake kutoka kijiji kimoja hadi kingine. Baada ya kumaliza ziara ya Kiteto, msafara huo umeelekea Wilaya ya Babati.

No comments:

Post a Comment