NA MWANDISHI WETU
WADAU wa kilimo duniani wametumia mkutano wa kimataifa wa haki za
wakulima kujadili namna kifungu cha tisa cha Mkataba wa Kimataifa wa
Rasilimali za Vyakula na Kilimo (ITPGRFA), unavyoweza kushughulikia
changamoto wakati wa dharura, ikiwamo misukosuko ya kisiasa na
majanga ya asili.
Katika mkutano huo wa pili uliofanyika hivi karibuni jijini Manila,
Ufilipino, taasisi zisizo za Serikali nchini, ziliwakilishwa na mtaalamu wa
sera na utafiti kutoka Mtandao wa Baionuai (TABIO), Daud Manongi.
Manongi alisema mkutano huo pamoja na mambo mengine, hoja ya
dharura kuhusu mustakabali wa wakulima ilitawala mijadala.
Alisema katika mjadala huo, mataifa yaliyotajwa kuathiriwa na
misukosuko ya kisiasa ni pamoja na Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Myanmar na Haiti.
Mtaalamu huyo alisema athari za majanga ni vimbunga, ukame na
milipuko ya visumbufu vikijadiliwa kama changamoto kubwa
zinazohatarisha ustawi wa wakulima.
“Kwa mujibu wa hoja hiyo, dharura hizi zimekuwa zikisababisha,
uharibifu wa mifumo ya mbegu na mazao, kupotea kwa maarifa ya jadi
ya kilimo, wakulima kushindwa kuhifadhi, kutumia, kubadilishana na hata
kuuza mbegu kipindi ambacho wanazihitaji zaidi,” alisema.
Alisema bila mikakati mahsusi, urejeshaji wa mifumo hii huchukua muda
mrefu na mara nyingi hukosa usawa, jambo linalosababisha ukosefu wa
haki kwa wakulima wadogo.
“Katika majadiliano hayo, ilisisitizwa kuwa ni lazima kuwe na malengo ya
moja kwa moja, yanayolenga kuwezesha urejeshaji haraka wa uzalishaji,
kuimarisha benki za mbegu za kijamii, kulinda na kudumisha maarifa ya
jadi ya wakulima,” alisema.
Alisema Sekretarieti ya Mkataba wa ITPGRFA ilikubali kuwa mfuko wa
dharura upo, lakini ikabainisha kwamba bado kuna haja ya kuanzisha
malengo yanayoakisi mazingira halisi ya dharura, na kushirikisha jamii
kikamilifu, ili wajisikie kuwa sehemu ya utekelezaji wa haki zao.
Manongi alisema mjadala huo umeonesha dhahiri, kuwa mustakabali wa
haki za wakulima nyakati za dharura, unategemea uwepo wa mikakati
thabiti na jumuishi, itakayowezesha wakulima kuendelea kuwa walinzi wa
urithi wa mbegu na maarifa ya kilimo duniani.
No comments:
Post a Comment