NA MWANDISHI WETU
WAUMINI wawili wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania wameiandikia rasmi Vatican wakiomba kufanyika kwa uchunguzi wa kichungaji na kiutawala kuhusu mwenendo wa Padri Dkt. Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Waumini hao, Stanslaus Thobias Nyakunga na Elia Phaustine Kabote, wamewasilisha barua yao kwa Balozi wa Vatican nchini, Archbishop Angelo Accattino, wakieleza wasiwasi wao juu ya tuhuma na mitazamo iliyoenea katika jamii kwamba Padri Kitima amekuwa akihusishwa na masuala ya siasa, hususan ndani ya chama cha CHADEMA.
Kwa mujibu wa waumini hao, madai hayo yawe ya kweli au la yameanza kuzua sintofahamu miongoni mwa waumini na kuliweka Kanisa katika hatari ya kutafsiriwa kama linaegemea upande wa kisiasa, hali ambayo inaweza kudhoofisha nafasi yake kama taasisi ya amani, upatanisho na mwongozo wa kimaadili.
Katika barua hiyo, Nyakunga na Kabote wamesisitiza kuwa hawakusudii kutoa hukumu binafsi dhidi ya Padri Kitima, bali wanaiomba mamlaka ya Kanisa kulishughulikia suala hilo kwa busara ya kichungaji ili kulinda umoja wa waumini na taswira ya Kanisa mbele ya jamii.
Waumini hao pia wamerejea maandiko ya Biblia, wakikumbusha wajibu wa viongozi wa Kanisa kuwa nguzo za amani na maridhiano, wakinukuu Mathayo 5:9 inayosema “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu,” pamoja na 1 Wakorintho 14:33 inayosisitiza kuwa Mungu ni wa amani, si wa machafuko.
Hatua hiyo inakuja wakati taifa likiwa katika mjadala mpana wa kisiasa na kijamii, ambapo taasisi za dini zinatarajiwa kuendelea kuwa nguzo za utulivu, mshikamano na maridhiano ya kitaifa.
Katika barua yao, waumini hao wameomba kufanyika kwa uchunguzi wa mwenendo wa Padri Kitima, kutolewa kwa mwelekeo wa wazi unaohakikisha Kanisa linabaki huru dhidi ya siasa za vyama, pamoja na kuchukuliwa kwa hatua zitakazolinda umoja wa waumini na mamlaka ya kimaadili ya Kanisa.
Waumini hao wamesema wanaiamini Holy See kuwa na busara na mamlaka ya kushughulikia suala hilo kwa maslahi mapana ya Kanisa na jamii kwa ujumla.





No comments:
Post a Comment