NA MWANDISHI WETU
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Singapore zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara, uwekezaji, maendeleo ya vijana, uchumi wa kidijitali na usalama wa chakula kufuatia mazungumzo ya kihistoria yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ziara ya kwanza kabisa ya kiserikali ya Rais wa Singapore, , nchini Tanzania, hatua ambayo pia imeadhimisha miaka 45 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Akizungumza baada ya mazungumzo rasmi, Rais Samia alisema Tanzania na Singapore zimefanya tathmini ya ushirikiano uliopo na kukubaliana kuupanua zaidi ili kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wa nchi zote mbili.
Alisema kiwango cha sasa cha biashara kati ya Tanzania na Singapore kinakadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 299 huku Singapore ikiwa na miradi 36 ya uwekezaji nchini Tanzania, kiwango ambacho hakilingani na ukubwa wa urafiki uliopo kati ya mataifa hayo.
"Tumekubaliana kuongeza biashara na uwekezaji kwa kutumia mikataba mbalimbali tuliyosaini leo kama msingi wa kufungua fursa mpya za kiuchumi kati ya nchi zetu," alisema Rais Samia.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili pia mikakati ya kuwawezesha vijana kupitia elimu, mafunzo ya ujuzi, ubunifu na ujasiriamali, huku Tanzania ikieleza dhamira yake ya kuwashirikisha vijana kikamilifu katika utekelezaji wa mkakati wa uchumi wa kidijitali unaotarajiwa kutekelezwa kati ya mwaka 2024 na 2034.
Rais Samia aliikaribisha Singapore kuwekeza katika sekta ya kilimo nchini kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula na kuimarisha usalama wa chakula, akieleza kuwa Tanzania ina ardhi na rasilimali zinazoweza kusaidia utekelezaji wa mpango wa Singapore wa kuhakikisha upatikanaji wa chakula kutoka mataifa mbalimbali.
Kwa upande wake, Rais Tharman alisema dunia inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kimazingira yanayohitaji ushirikiano wa karibu zaidi kati ya mataifa ya Afrika na Asia.
Alisema Singapore inaiona Tanzania kama lango muhimu la biashara katika Afrika Mashariki kutokana na nafasi yake ya kimkakati katika Bahari ya Hindi na ukuaji wake wa kiuchumi.
Rais huyo aliunga mkono dhamira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanza mazungumzo kuelekea makubaliano ya biashara huria na Singapore, akisema hatua hiyo itafungua masoko mapya kwa bidhaa na huduma kutoka pande zote mbili.
Aidha, alisema Singapore iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maendeleo ya ujuzi kwa vijana, huduma za afya, utafiti wa kisayansi, maendeleo ya viwanda, miundombinu ya biashara na usimamizi wa maeneo maalumu ya kiuchumi.
Wakati wa ziara hiyo, Tanzania na Singapore zilisaini mikataba na hati tano za makubaliano katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuondoa kodi mara mbili, maendeleo ya ujuzi, biashara ya kaboni, mashauriano ya kidiplomasia na uwezeshaji wa biashara.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni makubaliano ya kuondoa utozaji kodi mara mbili na kuzuia ukwepaji wa kodi, hati ya ushirikiano katika maendeleo ya ujuzi kwa watumishi na vijana, makubaliano ya biashara ya kaboni chini ya Mkataba wa Paris, mfumo wa mashauriano kati ya wizara za mambo ya nje za nchi hizo mbili pamoja na makubaliano ya kukuza biashara na uwekezaji.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa hatua muhimu ya kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore, huku viongozi wa mataifa hayo wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha biashara, uwekezaji na maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wao.








No comments:
Post a Comment