Hery Samir ‘Blue’: - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, February 9, 2012

Hery Samir ‘Blue’:

Mkali wa staili anayebadilika kila kukicha
-        Alianza kufoka, sasa anaimba
- Rangi ya blue inamng’arisha zaidi


Na Asmah Mokiwa
MUZIKI wa kizazi kipya unaojulikana kama Bongo Fleva unazidi kukua siku hadi siku nchini, ambapo ndivyo wasanii wanavyozidi kuwa wabunifu.

Wapo wasanii wengi wanaoibuka na kushika chati na kupata umaarufu kisha kupotea, na wengine kuzidi kusonga mbele.

Pengine hili limekaa vyema kwa nyota wa miondoko ya RnB na Bongo Fleva, Herry Samir ‘Blue’ ambaye aliibuka akiwa na umri mdogo na bado ni tishio kwa wasanii wengine wakubwa.

Blue ambaye aliyekuwa akijiita Lil Sama, alipachikwa jina hilo la Blue na mashabiki wake baada ya kibao chake cha kwanza kilichokonga nyoyo za mashabiki wake kilichokuwa kinajulukana kama ‘Mr Blue’.

Wimbo huo wa Mr Blue alimtambulisha vyema kwa kuinadi rangi ya blu jinsi inavyopendeza kwa kila kitu haswa katika mavazi.

Blue ambaye pia kwa sasa anajiita Kabayser  aliingia katika tasnia hiyo kwa staili ya kufokafoka, ambapo alifanya vyema katika wimbo wake wa kwanza uliomtambulisha wa Mr Blue.

Katika kuwasoma mashabiki wake, Kabayser alibadilisha staili ya uimbaji na kuingia katika staili ya RnB, ambapo amefanya vyema katika nyimbo zake mbalimbali alizoimba.

Mbali na nyimbo ya ‘Mapozi’ na ‘Inaniumiza’, moja kati ya nyimbo zake zilizokonga nyoyo za mashabiki wake ni pamoja na ‘Tabasamu’ aliyoimba kwa kumshirikisha mkali wa RnB nchini, Steve RnB.

Msanii huyo mwenye malengo ya kuwa Injinia, aliimba nyimbo hiyo kwa staili yake mpya ya uimbaji ambayo hadi sasa anitumia katika nyimbo zake.

Mbali na hilo aliweza kufanya ziara mbalimbali za kimuziki, hali iliyomfanya kujulikana ndani na nje ya nchi.

Moja kati ya ziara alizofanya ni pamoja na ile ya  kimuziki bara la Ulaya na Afrika nzima, ambapo aliporudi alizindua video yake  ya ‘Tuko Pamoja’, aliyoifanya nchini sambamba na kuangusha shoo kali ndani ya Ukumbi wa Club Bilicanas mwanzoni mwa mwaka huu.

Hery Samir 'Mr Blue'
    
Katika uzinduzi huo, alifanikiwa kurudisha heshima yake upya kwa mashabiki wake kwani hadi sasa, video hiyo inafanya vyema katika chati mbalimbali za muziki nchini.

Uzinduzi huo aliufanya vyema kwa kuwakumbusha mashabiki albam zake mbili zikiwemo za ‘Mr.Blue’ na ‘Yote Heri’.

Mr Blue ni moja kati ya wasanii wa kuigwa, kwani ana utofauti wa uimbaji na anabadilika kadri siku zinavyoenda.

Pia, anasifa ya kuwa mbunifu katika video za nyimbo zake, kwani hata katika video aliyeshirikishwa na mwanadada mkongwe katika fani hiyo, Judith Wambura ‘Jide’ ya ‘Wangu’ inadhihirisha ubunifu wake.

Baada ya kutamba na  nyimbo zake nyingi za ujumbe wa mapenzi na majigambo, anatamba na ngoma yake mpya inayozungumzia pombe za mwisho wa wiki iitwayo  'Tilalilah'.

Ukiangalia video yake ya ‘Tabasamu’ unaweza ukasema sio Tanzani,a ni msanii wa mbele jinsi alivyoweza kuipamba video hiyo.

Blue alizaliwa miaka 23 iliyopita katika  Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Alichukua elimu yake ya msingi mkoani mwanza na kuchukua elimu yake ya Sekondari katika shule ya Bwilu iliyoko mkoani humo.

No comments:

Post a Comment