JKT Ruvu 'kuvunja benki' kwa usajili
Na Charity James
UONGOZI wa timu ya soka ya JKT Ruvu uko katika mipango ya kuhakikisha unafanya usajili wa nguvu katika kipindi hiki kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao.
Akizungumza na Magendela Blogspot Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa JKT Ruvu, Masau Bwire, alisema viongozi wa timu hiyo wako katika mikakati hiyo ili kukiimarisha kikosi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.
"Kwa ujumla timu ya JKT Ruvu iko katika mikakati mizito ya usajili, ukizingatia kuwa ligi imekwisha, kilichobaki ni kuandaa timu kwa ajili ya msimu ujao, hivyo mikakati ni kuongeza vijana wazuri ili wasaidiane na waliopo," alisema Bwile.
Alisema timu hiyo imeamua kufanya usajili wa nguvu kwani wanahitaji timu yao kushika nafasi za juu za Ligi Kuu Vodacom msimu ujao, na ikiwezekana nao waiwakilishe nchi katika michuano ya kimataifa ikiwemo Kombe la Shirikisho na lile la Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Lengo la kufanya usajili mzuri ni kuhakikisha timu yetu inashika nafasi za juu katika michuano hii msimu ujao, na hapa kuna kazi nzito kama hatutaanza mapema kujiwekea mikakati madhubuti," alisisitiza Bwire.
Alisema JKT Ruvu imekuwa bora tangu kujiunga na Ligi Kuu, kwani imekuwa ikionesha upinzani mkubwa kwa timu zote zilizokutananazo lakini wameshindwa kushiriki mashindano makubwa.
Wednesday, May 23, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment