WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa
ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha
mradi huo unajengwa kwa viwango na kukamilika kama ilivyobainishwa
kwenye mkataba.
Amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo unaendelea
vizuri katika vipande vyote na kwamba Serikali itahakikisha mradi huo
haukwami na itakabiliana na viashiria vyote vinavyoweza kukwamisha
utekelezaji wake.
Ameyasema hayo jana, Alhamisi, Novemba 24,
2022 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa stesheni kuu ya Dodoma
katika eneo la Mkonze, jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya
kukagua maendeleo ya ujenzi wa stesheni hiyo, Mheshimiwa Majaliwa
amewataka Watanzania wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi huo wasimamie
usalama wa mradi na wawe walinzi ili ukamilike kama ilivyokusudiwa.
Aidha,
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassam inaendelea kufanya maboresho kwenye
sekta mbalimbali ikiwemo ya usafirishaji.
“Rais Samia anaendelea
na mkakati wake wa ujenzi wa reli, endeleeni kuwa na imani na Serikali
yenu, lengo lake ni kuhakikisha anainua uchumi wa mtu mmoja mmoja na
Taifa kwa ujumla”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkurugenzi
wa Jiji la Dodoma kuwa na mkakati wa maeneo ya uwekezaji kutokana na
fursa ya ujenzi wa reli hiyo ikiwemo ujenzi wa kituo cha mabasi jirani
na stesheni hiyo.
Kwa upande wake, Mkurgenzi Mkuu wa Shirika la
Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema kuwa Shirika hilo lipo
kwenye mpango wa ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa ya mizigo.
“Hadi sasa TRC imesaini mkataba wa ununuzi wa vichwa vya treni vya umeme
19, seti za treni 10 zenye uniti 80.”
Amesema pia shirika hilo
itanunua mabehewa ya kawaida ya abiria 89, mabehewa ya ghorofa 30 ambayo
yanakuja, mabehewa ya mizigo 1,430 na vifaa vya matengenezo 26.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) ya Dodoma katika eneo la Mkonze jijini Dodoma,

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) iliyopo eneo la Mkonze jijini Dodoma,

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC, Profesa John Kondoro (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika eneo la Mkonze jijini Dodoma,

Baadhi ya mafundi waoshiriki katika ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika eneo la Mkonzi jijini Dodoma wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao baada ya kukagua ujenzi huo,

Muonekano wa Jengo la Makao Mkuu ya Shirika la Reli Tanzania TRC jijini Dodoma ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokagua ujenzi wake jana, Novemba 24, 2022. Mheshimiwa Majaliwa pia alikagua ujenzi wa Setesheni Kuu ya Reli ya Kisasa SGR katika eneo hilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment