Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya
Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), baadhi ya Menejimenti ya TFRA na watumishi
wa Kiwanda cha ABM cha Tanga walipotembelea eneo la Machimbo ya Madini
yanayotumika kutengeneza Visaidizi vya Mbolea kiwandani hapo.
NA MWANDISHI WETU
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Tanga, Wakili Mnyema, ametoa wito kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuendelea kushirikiana na ofisi yake katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa wananchi wa mkoa huo ili waongeze tija kwenye uzalishaji.
Pia, Mkurugenzi wa Bodi ya TFRA, Thobias Mwesigwa, amesema elimu ya umuhimu wa matumizi ya mbolea unaeleweka zaidi kwa wamiliki wa viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo huku baadhi ya watumiaji hawana elimu ya kutosha kuhusu hilo na kusababisha mwitikio mdogo wa kutumia mbolea kwenye kilimo.
Kulingana na changamoto hiyo, ameahidi kazi kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha wazalishaji, Menejimenti na Ofisi za mikoa zinashirikiana katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea.
Naye, Mkurugenzi Hadija Jabiri, ameiomba serikali kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya mbolea katika Mkoa wa Tanga na kueleza uzalishaji ukiwa mkubwa utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mbolea nchini na kupunguza utegemezi wa kuagiza mbolea nje ya nchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Gothard Liampawe, Meneja wa TFRA Kanda ya Kaskazini amesema pamoja na Mkoa wa Tanga kuongoza kuwa na viwanda vingi vya uzalishaji wa mbolea na visaidizi vya mbolea bado mkoa huo umekuwa changamoto kwenye matumizi ya mbolea pamoja na elimu inayoendelea kutolewa.
Amesema TFRA imejitahidi kuondoa changamoto ya usambazaji wa mbolea iliyojitokeza msimu wa kilimo wa 2022/2023 kwa kuvitumia vyama vya ushirika vilivyotayari kushiriki katika kusambaza mbolea na tayari vyama hivyo vimepewa mafunzo ya uuzaji wa mbolea kwa kwa kutumia mfumo wa kidigitali ulioboreshwa.
Wajumbe hao walitembelea viwanda viwili vya uzalishaji wa mbolea na visaidizi vya mbolea ambavyo ni Neelkanth Chemmicals LTD na ABM na kushauriana namna bora ya kuhamasisha matumizi ya bidhaa wanazozizalisha, pamoja na kuheshimu Kanuni, Sheria na miongozo inayosimamia tasnia ya mbolea nchini.
CR - DARUBINI YA HABARI BLOG
No comments:
Post a Comment