NA
JOHN MAPEPELE
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed
Mchengerwa ameitaka Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),
kwenda kuondoa utendaji wa mazoea ili kuweka misingi ambayo itaifanya Tanzania
kuwa namba moja Afrika na dunia katika sekta ya utalii.
Mchengerwa ametoa kauli hii leo Agosti 21,
2023 jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii
Tanzania (TTB) na Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Aidha, ameitaka Bodi ya TTB kukaa na Menejimenti
ili kufanya mapitio ya Sheria ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya
utalii.
Waziri Mchengerwa ameitaka Bodi kwenda kutatua mara moja changamoto zilizopo na kusimamia mikakati ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ambapo amefafanua kuwa idadi ya vivutio vilivyopo nchini hailingani na mapato yanayopatikana.
Amesema bila utangazaji madhubuti unaokwenda sambamba na utoaji wa huduma bora kwa watalii, taifa haliwezi kunufaika na rasilimali za utalii zilizopo nchini hata kama uhifadhi wa rasilimali hizo utaimarishwa.
Amempongeza Rais kwa maono yake ya kuifungua na
kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kupitia filamu ya The Royal Tour
“Ni katika muktadha huo, Mheshimiwa Dkt. Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliamua kutufungulia
njia kwa kuanzisha Programu maalum ijulikanayo kwa jina la Tanzania: “The Royal
Tour’’ inayolenga kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji. Hivyo,
tunao wajibu wa kuhakikisha kuwa Programu hiyo inakuwa endelevu sambamba na
kuanzisha mikakati mbalimbali itakayochochea ongezeko la watalii hapa nchini
pamoja na mapato yatokanayo na Sekta ya Utalii”. Amefafanua Mhe. Mchengerwa
Kwa upande wa Bodi ya TANAPA, ametoa wito kwa Bodi
ya kuendelea kusimamia mfumo wa kijeshi ili kuweza kufikia malengo ya
kuanzishwa kwa Jeshi la Uhifadhi hususani katika eneo zima la uhifadhi wa
rasilimali za Wanyamapori na Misitu katika maeneo ya hifadhi zote.
Amewahimiza kujikita katika utatuzi wa migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu. Pia, kuhakikisha kuwa migogoro yote iliyopo kati ya Wananchi na Hifadhi inapatiwa suluhisho la kudumu na kuzuia kutokea kwa migogoro mipya ili uhifadhi endelevu uweze kupatikana.
Ameiwataka wajumbe wa bodi hiyo kushirikiana na
wadau wote wa uhifadhi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika
kutekeleza majukumu yao na kusisitiza kutorudi nyuma katika uhifadhi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe.Timetheo Mzava ametoa wito kwa bodi hizo
kufanya kazi kwa bidii.
Wenyeviti wa bodi hizo Jenerali (Mst.) George
Marwa Waitara-TANAPA na Mhe. Balozi, Dkt. Ramadhani Dau -TTB wamemshukuru Mhe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuteuliwa kuwa Wenyeviti wa Bodi
hizo na kumwahidi Mhe. Mchengerwa kufanya kazi kwa bidii.







No comments:
Post a Comment