NMB, ATCL ZAINGIA MAKUBALIANO YA KIBIASHARA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, August 16, 2023

NMB, ATCL ZAINGIA MAKUBALIANO YA KIBIASHARA


Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi (wa pili kushoto), wakionyesha mfano wa ndege kuashiria uzinduzi wa mfumo wa malipo ya tiketi za ndege kupitia matawi, mawakala wa NMB  katika hafla iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam Agosti 16, 2023. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha wa ATCL, Jamal Kiggundu na kulia ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi. (Na Mpiga Picha Wetu).




 NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wamezindua ushirikiano wa kibiashara wa mifumo ya malipo ya tiketi za ndege 'Anga Rafiki - Tiketi Yako Imebima,' unaowapa fursa wasafiri wa kulipia tiketi kupitia matawi, mawakala na huduma za NMB Mkononi App, ambazo zitakuwa zimekatiwa Bima ya Safari moja kwa moja.

Ushirikiano huo umezinduliwa Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam leo Jumatano Agosti 16, ambako msafiri atakayelipia tiketi za safari za ndani ya nchi kupitia NMB, atakatiwa bima ya maisha, ulemavu ama upotevu wa mizigo safarini, ambapo atalipwa hadi Sh. Mil. 5 za Kitanzania itapotokea mteja kufariki dunia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO), Ruth Zaipuna, alisema kwamba, kupitia matawi 229 na mawakala zaidi ya 21,000, wasafiri nchini wanaenda kufikiwa kirahisi kuwezesha upataji tiketi na kwa wateja wa benki hiyo wanazo njia za ziada za kulipia tiketi hizo kwa simu ya mkononi kupitia USSD na NMB App.

"Ni imani yetu sisi NMB kwamba, huduma hii sio tu inaenda kumpa urahisi na wepesi msafiri wa kulipia tiketi yake, bali kumkinga pia na majanga yatokanayo na safari kama ulemavu, kifo na upotevu wa mizigo.

"Mteja akilipia tiketi ya ATCL kupitia NMB, ikatokea akafariki - ingawa hatuliombei hilo, ama kupata ulemavu akiwa safarini, yeye ama wategemezi wake watalipwa hadi Sh. Milioni 5.

"Na iwapo mzigo (checked in Baggage) wa msafiri utapotea, mteja wetu atalipwa Shilingi 300,000, lakini pia ikiwa safari itasogezwa ama kuahirishwa, atalipwa Shilingi 150,000. Bima hizi tutazilipa kupitia washirika wetu Kampuni ya Reliance Insurance," alifafanua Zaipuna.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi, aliipongeza NMB sio tu kwa ushirikiano wao huo, bali kuweka ziada ya Bima ya Safari kwa wateja wao, huku akibainisha kwamba hakuna tena sababu ya Watanzania kusafiri kwa hofu wakati kuna ATCL na NMB.

No comments:

Post a Comment