NA MAGENDELA HAMISI
STAA wa muziki wa dansi nchini, Johnson Nguza maarufu kwa jina la Papii Nguza, na wakung’uta gitaa wawili wametangazwa rasmi kujiunga na bendi ya Town Classic inayoongozwa na Mkurugenzi wake, Patric Kessy.
Akiwatangaza leo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi Kessy ametanabaisha kuwa lengo la kuwaongeza wanamuziki hao ni kuhakikisha kundi hilo ambalo lina mwaka tangu kuanzishwa kwake linakua na nguvu na kuhimarika kimuziki sanjari na kuwa gumzo mjini.
“Baada ya mazungumzo marefu na wanamuziki hawa, tunayofuraha kubwa leo kuwatambulisha katika bendi yetu na kuanzia sasa hawa ni wanamuziki wetu na tayari tumeingia nao mikataba na wako tayari kufanya kazi.
“Kama kuna mtu tumemkosea kwa ujio wa wanamuziki hawa tunamuomba radhi ni yetu ni njema na si kuleta vurugu katika tasnia ya muziki wa dansi, baada ya utambulisho wa leo, wataanza kupanda jukwaani Septemba tisa mwaka huu katika ukumbi wa Makumbusho jijini Dar es Salaam na tunawakaribisha mashabiki wote,” amesema.
Wanamuziki wengine wawili ambao Mkurugenzi Kessy, aliwatambulisha ni mpiga gitaa la solo, Elombe Kichinja na mpiga gitaa zito, ‘Baba Base’.
Mkurugenzi Kessy ameongeza kuwa wamefanya mengi katika tasnia hiyo na wanachoendelea nacho ni kurejesha hadhi ya muziki wa dansi ambao unaonekana kuyumba na kupoteza mvuto wake.
Kwa upande wake Papi Kocha akizungumzia kutua kwake katika kundi hilo, amesema kuwa anafuraha kubwa kujiunga na kundi hilo hilo kwa maana ni sehemu sahihi zaidi.
“Namshukuru Mungu kwa kuendelea kuniweka salama na afya njema, pia nimshukuru mke wangu kunipa furaha ya moyo, kikubwa ambacho naweza kusema nimefurahi kujiunga katika kundi hili kwa maana ni sehemu sahihi na kule nilipotoka nimeaga vizuri na ninachoweza kusema tupo tayari kufanya kazi na tayari tumeandaa nyimbo mbili na baada ya miezi sita tutaachia albamu,” amesema
Mkali huyo katika tasnia hiyo ambaye aliwahi kuwika na kibao kinachoitwa Seya, ametamba kuwa mashabiki wakae mkao wa kula burudani na wajitokeze kwa wingi katika maonesho yao.





No comments:
Post a Comment