*YAELEKEZA MKAKATI WAKE WA KUENDELEZA MGODI WA MAKAA YA MAWE
*VITUO VYA MFANO VYATAJWA KUONGEZA TIJA, WATAKA VIONGEZEWE
UWEZO
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeieleza
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa linamiliki idadi ya Leseni
143 za uchimbaji madini ya aina mbalimbali zikiwemo leseni Mpya 3 za Madini ya
Kimkakati ya Lithium, Graphite na Rare Earth Elements pamoja na kueleza
utekelezaji wake.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji
wa STAMICO, Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala Deusdedith
Magala Agosti 22, 2023 katika kikao cha Kamati jijini Dodoma, amesema
kwamba, miongoni mwa leseni hizo, zipo zinazoendelezwa na Shirika,
Kampuni Tanzu na ubia na kuongeza kuwa, Shirika linamiliki leseni ambazo zipo
hatua mbalimbali za utafiti.
Akizungumzia leseni zilizo katika hatua ya utafiti
ambazo zinahitaji uwekezaji, Magala amesema ni pamoja na zilizomo katika madini
ya dhahabu, limestone, rubi, tin, nikeli, manganese, lithium, colbat, phosphate
na copper.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati
hiyo Judith Kapinga ametoa ushauri kwa STAMICO kutafakari upya
kuhusu mpango wake kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na
wawekezaji wa kuwekeza katika uzalishaji wa umeme wa Megawati 200 badala
yake lifikirie kuzalisha kiwango kikubwa zaidi ili kukidhi mahitaji ya nishati
ya umeme nchini na kuzingatia kuanzisha miradi yenye sura ya kitaifa.
Aidha, kwa upande wa wajumbe wa Kamati hiyo, mbali
na kulipongeza Shirika hilo kutokana na juhudi kubwa iliyofanywa ya kuendeleza
Sekta ya Madini ikiwemo kuwaendeleza wachimbaji wadogo, wameitaka STAMICO
kuviongezea uwezo vituo hivyo ikiwemo kuongeza idadi yake kutokana na mahitaji
ya watumiaji kwa lengo la kuongeza tija na kurahisisha shughuli za wachimbaji
wadogo wa madini kutokana na matokeo yenye tija ambayo yamepatikana kupitia
vituo hivyo.
Vituo vya mfano vilianzishwa kwa lengo la kutoa
mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji bora na wa kisasa wa madini usioathiri
mazingira na unaohamasisha matumizi ya teknolojia rahisi katika shughuli za
uchimbaji mdogo. Hivi sasa kuna jumla ya vituo vitatu vya mfano vilivyoko
katika maeneo ya Lwamgasa na Katente mkoani Geita na Itumbi wilayani Chunya.
Wakati akisoma hotuba yake Bungeni mwezi Aprili,
2023, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko alisema katika kipindi cha
Julai, 2022 hadi Machi, 2023 jumla ya gramu 30,475.72 za dhahabu zenye thamani
ya shilingi bilioni 3.6 zilizalishwa kupitia vituo hivyo na kiasi cha shilingi
milioni 279.6 zililipwa Serikalini.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa
Madini Dkt. Steven Kiruwa amesema wizara imepokea ushauri wote uliotolewa na
itaufanyia kazi ikiwemo kuisimamia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini
Tanzania (GST) kufanyia utafiti leseni zinazomilikiwa na STAMICO.
STAMICO lilianzishwa mwaka 1972 likiwa na jukumu
la kushiriki na kuendeleza rasilimali za madini nchini kwa niaba ya Serikali.
Mwaka 2015, shirika lilifanyiwa maboresho kupitia Public Corporation (Establishment)
(Amendment) Order iliyolenga kulifanya kuwa chombo madhubuti cha
kuwekeza kimkakati katika Sekta ya Madini kupitia miradi mbalimballi ili
kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa.
Miongoni mwa majukumu ya STAMICO ni kuwekeza
kwenye miradi ya kimkakati ya utafutaji na uchimbaji madini; kuwekeza katika
shughuli za uchenjuaji; uongezaji thamani madini na uuzaji madini; kutoa huduma
za kibiashara za uchorongaji miamba na utafutaji wa madini;
Majukumu mengine ni kutoa huduma za ushauri wa
kitaalam na kiufundi katika Sekta ya Madini zikihusisha ushauri wa kijiolojia,
kihandisi, mazingira pamoja na uandaaji wa upembuzi yakinifu wa miradi ya
uchimbaji au uongezaji thamani madini na kuratibu uendelezaji wa
wachimbaji wadogo nchini kwa kutoaushauri wa kitaalam kwa wachimbaji hao.
No comments:
Post a Comment