Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt Angeline Mabula akiwasili ofisi za CCM wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe wakati wa ziara yake mkoani humo mwishoni mwa wiki. Kulia kwa Dkt Mabula ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba.
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha
Mapinduzi (MNEC) Dkt Angeline Mabula, amewataka wanachama wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) kutangaza mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita ili yaweze kufahamika
kwa wananchi.
Dkt Mabula ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi amesema hayo tarehe 11 Agosti 2023 alipotembelea ofisi
ya CCM wilaya ya Ludewa na kuzungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama
hicho akiwa katika ziara yake Mkoa wa Njombe.
Alisema, wakati serikali ya awamu ya sita
ikifanya mambo makubwa ya kuwaletea watanzania maendeleo, viongozi pamoja na
wanachama wa CCM katika ngazi mbalimbali wana jukumu la kutangaza mafanikio
yaliyofanywa na serikali inagoongozwa na Raisi Samia Suluhu Hassa.
"Chama kitangaze mafanikio ya serikali na
ninyi viongozi wa ngazi mbalimbali mnalo jukumu hilo ambapo Rais wetu Samia
Suluhu Hassan ameonesha kuwajali wananchi kwa ujenzi wa madarasa, zahanati
pamoja na kuanzizsha shule mpya, hayo ni mafanikio makubwa" alisema Dkt
Mabula.
Kwa mujibu wa Mjumbe huyo wa halmashauri kuu ya
Taifa ya CCM, yote yanayofanywa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kiasi kikubwa yamemgusa kila mtu kutokana na kulenga huduma za jamii.
Dkt Mabula pia amegusia miradi mikubwa ya kimkakati kama vile Bwawa la Mwalimu
Nyerere pamoja na reli ya mwendo kasi kuwa ni miradi inayokwenda kuipaisha
Tanzania ambapo amesema hata mchakato wa bandari unaoendndelea sasa
utakapokamilika unaenda kuwa wa aina yake.
Aidha, amekitaka chama cha Mapinduzi wilaya ya Ludewa kuangalia fursa za
uwekezaji katika miradi mbalimbali na kutolea mfano wa Liganga na Mchuchuma
kuwa chama kinaweza kuwekeza katika eneo hilo ili kukiwezesha kutekeleza
majukumu yake bila kutegemea misaada.
"Ni vizuri chama kikaangalia fursa zinazopatikana, kama hapa mnao mradi wa
Liganga na mchuchuma mnaweza kuomba vitalu na kuwekeza ili chama kiwe na nguvu
na kujisimamia chenyewe jambo litakalowafanya kuheshimika na kama huwezi
kujisimamia siyo vizuri". alisema Dkt Mabula.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt Angeline Mabula akizungumza kwenye kikao na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho wilayani Ludewa mkoa wa Njombe mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva.




No comments:
Post a Comment