NGOME ya wanawake ya ACT Wazalendo, wametakiwa kujipanga na kujitokeza kupigania kuondelewa kwa nafasi ya Viti Maalum Bungeni ili kuisaidia Serikali kutopoteza fedha ambazo zingeweza kufanya mambo mengine ikiwemo kutatua kero za wananchi.
Hayo yamezungumzwa leo Machi 2, 2024 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba na Sheria (JUKATA), Dkt. Ananilea Nkya wakati wa Mkutano Mkuu wa Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo ambao umempitish,a Janeth Rithe kuwa mwenyekiti kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kwa kupata kura 65 sawa na asilimia 58. 8 huku Saveline Mwaijage akipata kura 46 sawa na asilimia 41.4.
“Tunapendekeza mfumo wa viti maalumu ufutwe ili kila mwanamke aende majimboni kugombea na nyinyi Ngome ya Wanawake ACT, pambaneni na kulisemea hili ili mkakati huu ufanikiwe jambo litakalosaidia Serikali, fedha zinazotumika kwa ajili ya kulipa wabunge ambao hawana majimbo zikafanye kazi nyingine za kijamii,” amesema.
Amesema kuwa zaidi ya shilingi 300 zinatumika kulipa wabunge ambao hawana majimbo hivyo ni vema jambo hilo likapigiwa kelele ili kuokoa fedha hizo ambazo kimsingi zinaweza kufanya mambo makubwa kwa ajili ya wananchi kutatua changamoto zao.
“Rais wetu ni msikivu na mkilisema hili na akalisikia, naamini anaweza kufanya mabadiliko katika jambo hilo, pazeni sauti ili kulifikisha suala hilo kwa Rais wetu mpendwa, sina shaka atalisikia tu na atafanya maamuzi,” amesema.
Dkt. Nkya pia ameisisitiza Ngome hiyo ya Wanawake ACT – Wazalendo kushawishi kwenye Kamati Kuu ya chama hicho ili watoe nafasi nyingi kwa wanawake kugombea kwenye uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za Mitaa na mwakani katika uchuguzi mkuu.
Amesema uongozi wa ACT wanauwezo wa kuwatengeneza wanawake ambao wanakuja kufanya vizuri katika chaguzi ikiwemo nafasi ya urais kama ilivyokuwa mwaka 2015 hivyo ni vema mchakato wa kutoa nafasi kwa wanawake kugombea ukaendekea kufanyiwa kazi ili kuleta mabadiliko kwa taifa.
Pia alisema kuwa wakati Tanzania inaingia kwenye mfumo wa vyama vingi ilitakiwa kubadilishwa kwa katiba ili kutoa nafasi ya kuingizwa mfumo wa vyama vingi jambo ambalo halikufanyika na kusababisha kuwepo kwa changamoto nyingi nyakati za uchaguzi.
Amefafanua kuwa kutokana na hali hiyo ni vema ACT wakaona nafasi ya kupigania kupatikana kwa Katiba Mpya ili kutoa fursa ya kufanyika kwa mabadiliko yanayohitajika ili kukidhi mfumo wa vyama vingi kufanya vizuri.
No comments:
Post a Comment