NEEC WANAWAKE 5000 KUMPONGEZA RAIS SAMIA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, March 9, 2024

NEEC WANAWAKE 5000 KUMPONGEZA RAIS SAMIA

Katibu wa NEEC Beng'i Issa akizungumzia kuhusu taasisi za wanawake kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan

 

NA MWANDISHI WETU

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za wanawake hapa nchini kesho wameandaa hafla maalumu ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan ikiwepo pia kutambua umahiri wake wa kuwa mwanamke kinara kwa masuala ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira.


Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam  jana, Katibu Mtendaji wa  NEEC, BengI Issa hafla hiyo ambayo itahudhuriwa  pia na  Rais Samia itafanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee sambamba na kumpongeza kwa ujasiri na uthubutu wake.


“Hii ni fursa ya kipekee kwa wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kwenye  hafla hiyo maalumu ya kutambua kuwa Rais Samia Suluhu kuwa ni mwanamke kinara wa masuala ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira,” amesema.


Issa amesema Rais Samia kwa ujasiri wake mbali ya kuwa mwanamke kinara kwenye masuala nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira hapa nchini, amefanikiwa kuifungua nchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa pia.


“NEEC inatambua na kuheshimu mchango wa Rais Samia katika kuwawezesha wanawake kutoka kwenye mazingira magumu ya nishati ya kupikia ikiwemo mkaa na kuni ambavyo  vimekuwa vikileta  madhara kwa afya ya binadamu na  mazingira hivyo kupitia mpango huo utaleta  matokeo chanya kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla wake,” alisema Bi. Issa.


Amesema kupitia mpango huo Rais Samia anatarajia kwenda Ufarasa kuongoza kikao ambacho kitawakutanisha marais wa dunia wakilenga  kumuunga mkono sambamba na kuja na mikakati itakayowezesha kukamilisha mpango utakaokuwa mwarobaini wa nishati safi ya kupikia na rafiki kwa mazingira.


Aidha, alibainisha kuwa Baraza linajumla ya  majukwaa  ya uwezeshaji  3,500 katika ngazi ya mtaa, vijiji, kata, wilaya, mikoa mpaka  ngazi ya kitaifa  lengo likiwa kuwaleta wanawake  wote pamoja  na kujadili na kuibua fursa  mbalimbali za kiuchumi na kutoa mchango kwa  maendeleo ya taifa.


“Majukwaa yote hapa  nchini yaende na kasi  ya mheshimimiwa Rais Samia ya kujielekeza  kwenye matumizi ya nishati safi na tuone kwamba hii ni fursa ambayo kila mwanamke wa kitanzania anatakiwa kuichangamkia sambamba  kuandaa miradi pamoja na kubuni rasilimali ambazo zinaendana na utunzaji wa mazingira,” amesema.  


Hafla hiyo  inatarajiwa kuwakutanisha wanawake  zaidi ya  5,000 kutoka  makundi mbalimbali  ya wanawake nchini  kama  majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi,  wanawake kutoka vyama vya utafiti , wanawake kutoka vyama vya makandarasi Tanzania, wanawake waandishi wa habari wanawake, wanawake kutoka kwenye vikoba, wanawake kutoka vyama vya kilimo na vyama vya utafiti.

No comments:

Post a Comment