NA MAGENDELA HAMISI, MOROGORO
WAKALA wa Usajili wa Leseni za Biashara (BRELA) hawawezi kumlinda mtu ama taasisi ambayo haijasajili jina la biashara ikiwa litasajiliwa na mwingine.
Hayo yamebainishwa leo, Juni 19 , 2024 mkoani Morogoro na Mkuu Wa Sehemu ya Kampuni kutoka Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara wa Brela,Lameck Nyange, wakati akiwasilisha mada inayohusu, Majina ya Biashara ( Sheria na Huduma baada ya kusajili), katika semina inayoendelea ya kuwaongezea uwezo waandishi kwaajili ya kuripoti kwa usahihi taarifa zinazohusu taasisi hiyo.
"Kumekuwa na changamoto kubwa kwa baadhi ya watu kuendesha shughuli zao bila kusajili jina la biashara, inapotokea mwingine anakuja kusajili jina hilo ambalo tayari lina mafanikio tunamsajilia, sheria inamlinda aliyesajili tu.
"Kwani lengo tunataka kila mwenye jina la biashara aje kusajili ili kupata ulinzi wa uhakika ikiwa atatokea mtu mwingine kutaka kusajili atashindwa," amesema.
Ameongeza kuwa na hata ikitokea mtu anatumia jina la biashara ambalo limesajiliwa Brela na akalalamikiwa, sheria madhubuti zitachukuliwa dhidi yake.
Kulingana na changamoto hiyo, ametoa wito kwa wafanyabiashara kusajili majina yao ya biashara ili kupata ulinzi dhidi ya watu watakaotumia jina hilo kinyume na utaratibu.
Alitoa mfano kuwa imekuwa ikitokea baadhi ya watu kuendesha biashara bila kusajili jina na mwingine anapofahamu hilo uwahi kusajili na kulilipia kila mwaka na mwenye jina anapotaka kusajili ushindwa kufanya hivyo na kuingia gharama zisizo za msingi kwa kufanya mazunguzo na aliyesajilli awali.
Aliongeza kuwa faida nyingine inayopatikana kwa aliyesajili jjna la biashara, mtu mwingine kutoweza kusajili jina linalofanana na hilo ikiwemo kimatamshi.
Pia ameongeza kuwa watu au taasisi ambazo zinashughulika na masuala ya kutafuta tenda watashindwa kufikia malengo yao ikiwa watakuwa hawajasaji jina la biashara na hata kushindwa kupata huduma za mikopo kutoka katika taasisi za fedha.
"Tunataka watanzania waelewe umuhimu wa kusajili jina la biashara ili kupata ulinzi kisheria kwa mtu atakayelitumia kinyume na utaratibu," amesema.
![]() |
No comments:
Post a Comment