UWEKEZAJI UJENZI WA RELI YA SGR WAFIKIA TRILIONI 23.3 - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, December 19, 2024

UWEKEZAJI UJENZI WA RELI YA SGR WAFIKIA TRILIONI 23.3


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji wa Serikali, Geryson Msigwa akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Desemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam.
.................................

NA DOTTO MWAIBALE

JUMLA  ya thamani ya uwekezaji katika ujenzi wa Reli ya SGR hadi sasa imefikia Dola za Marekani Bilioni 10.3 sawa na trilioni 23.3 ukiondoa kipande cha Uvinza hadi Musangati ambacho kipo katika hatua ya manunuzi

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji wa Serikali, Geryson Msigwa wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Desemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam.

”Kama mnavyofahamu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kupitia Shirika la Reli Tanzania inatekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia Dar es salaam hadi Mwanza na Kigoma. Mtandao wa reli umegawanyika katika kanda tatu ambazo ni Kanda wa Kati, Kanda ya Kusini na Kanda ya Kaskazini” alisema Msigwa.

Alisema kwa sasa ujenzi wa Reli kwa kiwango cha Standard Gauge unaendelea katika ukanda wa Kati ambapo utekelezaji wake unatekelezwa kwa awamu.

Alisema jumla ya thamani ya uwekezaji katika ujenzi wa reli hiyo hadi sasa imefikia Dola za Marekani Bilioni 10.3 sawa na trilioni 23.3.

Aidha, Msigwa alisema Wakandarasi wapo uwandani wakiendelea na kazi za ujenzi na usanifu kwa kipande cha Makutupora hadi Mwanza na Kigoma ambapo hadi kufikia mwezi Novemba, 2024 utekelezaji wake umefikia hatua ya kipande 3 Makutupora – Tabora Km 368 14.53% Kipande 4 Tabora – Isaka Km 165 6.27%, Kipande 5 Isaka – Mwanza Km 341 61.20%, Kipande 6 Tabora – Kigoma Km 506 7.16%, kipande 7 na 8 Uvinza – Musongati Km 280 Hatua ya Ununuzi.

Alisema  kipande cha Dar es salaam – Dodoma tayari uendeshaji umeshaanza.

Msigwa akizungumzia kuhusu utoaji wa huduma za Safari za Dar, Moro na Dodoma alisema toka kuanza kwa safari za treni hiyo ya ya umeme kati ya Dar, Moro na Dodoma, Juni 14, 2023 na kuzinduliwa kwa safari ya “Mchongoko’’ Novemba 1, 2024, huduma zimeendelea kuboreka na kwa sasa jumla ya ruti kumi (10) ambazo ni ruti nne (4) kutoka Dar es Salaam – Dodoma, Dodoma - Dar es Salaam pamoja na ruti mbili (2) kati ya Dar es Salaam – Morogoro.

Alisema hadi kufikia mwisho wa mwezi Novemba makusanyo yalikuwa ni Sh. Bilioni 30 na idadi ya abiria waliosafirishwa mpaka Desemba 11, 2024 ni milioni moja, laki moja na elfu sabini na nne, mia nne na nne ( 1,174,404) katika kipindi cha miezi minne tangu kuzinduliwa kwa njia za treni ya umeme kati ya Dar es Salaam na Dodoma mwezi Juni 2024 idadi ambayo ni mara mbili ya abiria waliosafirishwa na treni ya zamani (MGR), ambayo ilisafirisha jumla ya abiria 400,000 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Akizungumzia uimarishaji wa miundombinu ya treni na mikakati ya kutatua changamoto zinazijitokeza katika usafirishaji wa abiria Shirika la Reli Tanzania limeendelea kuboresha huduma zake ili kuhakikishaabiria wanafurahia zaidi kusafiri na treni ya umeme.

Msigwa alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema ambao wamekuwa wakihujumu miundombinu ya

treni kwa kufanya vitendo vya wizi wa nyaya na majaribio ikiwemo ukataji wa nyaya zinazoingiza umeme kwenye treni (catenary) hali ambayo imekua ikisababisha usumbufu kwa watumiaji wa usafiri huo.

Alisema Shirika la Reli Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vyetu vya usalama vimefanya kazi kubwa iliyopelekea kukamatwa kwa watu wanaofanya vitendo hivyo kama mlivyoona taarifa mbalimbali za jeshi la polisi na taratibu

za kuwafikisha mahakamani zinaendelea.

Alisema kuhusu ukamilishaji wa ujenzi wa reli katika awamu zilizobaki Makutopora –Tabora na  Isaka  Wakandarasi wapo uwandani na wanaendelea na kazi na wanatarajia kukamilisha ujenzi wa vipande vilivyobaki mwaka 2028. 

Msigwa akizungumzia Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL)

Alisema imeendelea kufanya vizuri katika biashara ya

usafiri wa anga kwa kusafirisha abiria na mizigo ndani na nje ya nchi hatua ambayo imeinua uchumi na kuiunganisha Tanzania na mataifa mengine.

Alisema uwepo wa ndege za kisasa 16 (Abiria 15 na mizigo1) zilizonunuliwa na Serikali umekua kichocheo katika kuboresha na kuimarisha sekta ya usafiri wa anga Tanzania.

Msigwa alisema mpaka sasa kampuni ya ndege Tanzania ina ndege Boeing 767 – 300F (Mizigo) 1, Boeing 737 – 9 Max 2, Boeing 787 – 8 (Dreamliner) 3, Airbus 220 – 300 4, DE Havilland Q400 5, DE Havilland Q300 1 na kueleza kuwa Ndege hizo zinafanya safari katika vituo 27 ambapo 15 ni vituo vya ndani ya

nchi (Mikoa) pia vituo vya nje ya nchi ikiwemo (Africa (9), Nje ya Afrika (3) - Dubai, Mumbai na Guangzhou)

Katibu Mkuu huyo alitaja mafanikio ya uendeshaji wa ndege hizo kuwa katika kipindi cha kutoka Januari mpaka Desemba 17, 2024, ATCL imefanikiwa kusafirisha abiria 1,109,803, mizigo tani 10,181 na kufanya safari za ndani na nje ya nchi 16,522.

Alisema Usalama na Utendaji  ATCL ina vibali vya usalama wa kufanya safari katika vituo takribani 12 vya nje ya nchi.

Aliongeza kusema kwamba  ATCL imeendelea kushirikiana na wataalamu wa ndani na nje ya nchi ikiwemo Kampuni za kuunda ndege (Boeing na Airbus) ambao wamekuwa wakisaidia kutoa mafunzo na kufanya mapitio ya uendeshaji wa shughuli zake kwa kuzingatia taratibu za usalama.

“ATCL imeendelea kufanya mashirikiano na mashirika makubwa ya ndege ikiwemo Emirate Airlines, Ethiopian Airline, Air India, Qatar, Airways, APG Airline, Hahn Air, Oman Air, Rwanda Air, Egypt Air, Proflight Zambia, LAM - Mozambique Airlines, na Fly Dubai, Ufufuaji wa ATCL umesaidia kukuza sekta mbalimbali ikiwemo utalii kwakutangaza vivutio vyetu na kuwawezesha watalii kufikia vivutio hivyo,” alisema Msigwa. 

Msigwa akizungumzia mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam alisema mradi huo ulibuniwa mwaka 2004 chini ya Halmashauri ya Jiji kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari barabarani Jijini Dar es Salaam.

Alisema gharama ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka kwa awamu zote sita inagharimu kiasi ya fedha za Marekani dola milioni 1,079.54.

Alisema Mpango Mkakati wa mradi umeainisha barabara ambazo zinajengwa kwa awamu sita (6) kama ifuatavyo:

Awamu ya Kwanza (KM 20.9): inahusisha barabara ya Morogoro

kutoka Kimara hadi Kivukoni pamoja na barabara ya Kawawa toka Magomeni hadi Morocco na Mtaa wa Msimbazi toka Fire hadi Kariakoo  ujenzi huo ulikamilika mwaka 2015 kwa asilimia 100 chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia. Miundombinu inatumika kwa uendeshaji wa mfumo wa BRT.

Alisema kwa sasa ujenzi unaendelea ili kuboresha usalama kwa kuongeza upana wa meta 3.5 kila uelekeo wa barabara sehemu ya Kimara hadi Ubungo, kutoka njia sita kwenda njia nane ili ifafanane na sehemu ya kutoka Kimara hadi Kibaha.

Aidha, Msigwa alisema Awamu ya Pili (KM 20.3) ni kutoka katikati ya mji  hadi Mbagala kupitia barabara za Sokoine, Gerezani, Bandari, Kilwa, Chang’ombe na Kawawa.

Alisema ujenzi huo ulikamilika kwa asilimia 100 mwezi Agosti 2024 kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kuwa miundombinu haijaanza kutumika.

Alisema Awamu ya Tatu (KM 23.3) ni kutoka katikati ya Jiji hadi

Gongolamboto kupitia barabara za Azikiwe, Bibi Titi, Nkrumah na Nyerere, pamoja na barabara za Lindi, Shaurimoyo, Uhuru na Mandela. 

Alisema ujenzi unaendelea kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na umefikia asilimia 65.81 na kuwa ujenzi wa Fungu la pili ambao ni ujenzi wa majengo,haujaanza, hivyo ni asilimia 0. 

Aidha Msigwa alisema  Awamu ya Nne (KM 29.13): kutoka katikati ya Jiji hadi Tegeta kupitia barabara za Bibi Titi, Ally Hassani Mwinyi na Bagamoyo,pamoja na sehemu ya barabara ya Sam Nujoma kutoka Mwenge hadi Ubungo ambapo ujenzi huo upo katika mafungu matatu.

Alitaja fungu la kwanza ni ujenzi wa Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kutoka makutano ya Bibi Titi na Mtaa wa Azikiwe, Barabara ya Bagamoyo kutoka Morocco hadi Mwenge, Daraja la Ubungo hadi Barabara ya Sam Nujoma zenye urefu wa kilomita 13.5 na kuwa ujenzi wa fungu hilo la kwanza la kwanza umefikia asilimia 9.2.

Alisema fungu la pili ni ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo kutoka Mwenge Kwenda Boko DAWASA yenye urefu wa kilomita 15.63. Hatua za ujenzi kwa fungu la pili ni zimefikia asilimia 15.2.

Msigwa alieleza kuwa fungu la tatu ni ujenzi wa Karakana mbili  Simu2000, Mbuyuni na Kivukoni ambao umefikia asilimia 3. 

Na kuwa Awamu ya Tano (KM 27.6) ni kutoka Ubungo hadi Bandari kupitia barabara ya Mandela na barabara ya Tabata toka Segerea hadi Kigogo na kuwa mradi huo upo hatua za manunuzi ya Makandarasi wa ujenzi  kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo wa Ufaransa (AFD).

Alisema Awamu ya Sita inatarajiwa kuhusisha barabara ya Mwai Kibaki (Moroko hadi Kawe, Kimara hadi Kibamba, Mbagala hadi Vikindu. 

Msigwa alitaja mafanikio kuwa utekelezaji wa mradi wa BRT umepata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na Uboreshaji wa huduma ya usafiri wa umma Dar es Salaam na kukuza ajira, Usafiri wa BRT umepunguza muda wa safari kutoka wastani wa

masaa matatu  kabla ya kuanza kwa huduma ya mabasi yaendayo haraka, hadi wastani wa dakika arobaini na tano (45).

Alisema hali hiyo imepelekea DART kupata tuzo ya Sustainable Transport Award 2018 na C40 Cities Bloomberg Philanthropies Award. Vilevile, mradi umetengeneza ajira za kudumu na za

muda. 

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kupunguza Msongamano wa Magari kwa kipindi ambacho idadi ya mabasi ilikuwa kubwa, mradi wa mabasi yaendayo haraka umepunguza msongamano kwenye njia ya magari ya kawaida ambapo baadhi ya watumiaji

wa magari binafsi wamekuwa wakitumia usafiri wa umma wa DART.

Aidha,usanifu na ujenzi wa miundombinu ya BRT umezingatia mahitaji ya watembea kwa miguu, watumiaji wa vyombo vingine vya usafiri visivyokuwa vya moto (non-motorized vehicles) na kuzingatia matumizi bora ya maeneo ya umma na

hivyo kupendezesha mandhari ya Dar es Salaam. 

Msigwa alitaja mafanikio mengine kuwa Mradi huo umekuwa wa Mfano Barani Afrika, umekuwa kivutio ndani na nje ya nchi.

“Tangu kuanzishwa kwa mradi takribani nchi 12 zilikuja

kujifunza zikiwemo nchi za Zambia, Zimbabwe, Uganda, Kenya, Ethiopia,Senegal, Ghana, Rwanda, Angola, Botswana, Nigeria, na Liberia,” alisema Msigwa.

Alisema mradi huo pia umepunguza Gharama za Usafiri  Baadhi ya wakazi wa Kimara walikuwa wakitumia takribani Sh.20,000 kwa kuweka mafuta kwenye magari yao kwa safari ya kwenda mjini na kurudi na pia kutumia takriban muda wa masa matatu  kufika mjini kati. Hivi sasa, wakazi hao wanatumia Sh.1,500 kama nauli kwa siku baada ya kuanza kutumia huduma za mabasi yaendayo haraka na wanatumia takriban dakika 45 kufika mjini kati. 

Alitaja mafanikio mengine kuwa kukuza Sekta Binafsi wa Uwekezaji wa Umma kwa Njia ya Ubia, (PPP) Uendeshaji na utoaji huduma za usafiri wa Umma kwenye mradi wa

DART unachochea ushiriki na uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) katika sekta ya usafiri.

Aidha, mfumo wa DART unatoa fursa na kuvutia wadau kutoka sekta binafsi kuwekeza kwenye ushoroba wa mfumo, huduma za usafiri wa umma, na kuendesha shughuli za kiuchumi katika mfumo.

Alisema kwa kutumia ubia kati ya sekta ya umma na sekta

binafsi imevutia wadau wa sekta binafsi kuingia ubia na Wakala wa DART kwa kuwekeza na huduma kwenye mfumo wa DART.

Aliongeza kuwa kueleza kuwa mradi huo umekuza matumizi ya teknolojia katika mifumo ya ukusanyaji wa nauli (GoT-AFCS) na

uongozaji wa mabasi (ITS) na kuwa Teknolojia hiyo inarahisisha huduma ya usafiri na inasaidia kuboresha na kutunza mazingira.

Msigwa alisema mnamo mwaka 2018, DART ilishiriki na kushinda shindano la kuboresha usafiri mijini uitwao Transformative Urban Mobility Initiative (TUMI) na kupewa ruzuku ya Euro 111,200. Wakala ulitumia tuzo hiyo kujenga mfumo wa kiganjani uitwao Mwendokasi App ambao unatumiwa na abiria kununua tiketi za DART kwa simu janja.

“Mfumo huu unamwezesha mtumiaji kupata taarifa za usafiri

zikiwemo umbali abiria alipotoka vituo vitatu vya karibu vya DART na muda atakaotumia kufika, hali ya usafiri na kutoa taarifa na matukio. Mfumo huo unapatikana kwenye App Store na Play Store. Aidha, Septemba 2, 2024, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa, Mh. Mohamedi Mchengerwa (Mb), alizindua matumizi ya kadi janja katika mfumo wa DART. 

Alitaja faida ya mradi huo ni kuthibiti Upotevu wa Mapato ya Nauli kwenye Mfumo na kuwa tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa kielektroniki wa kukusanya nauli (AFCS)

hususan matumizi ya kadi janja, kumekuwepo na uthibiti mkubwa wa upotevu wa mapato yatokanayo na nauli. 

Alisema mradi huo umesaidia kupunguza uchafuzi wa Mazingira na uzalishaji wa gesi chafu ya ukaa, ambayo ni mojawapo ya faida za kuanzisha mradi wa BRT ambapo kwa Dar es Salaam, usafiri wa umma umekuwa ukichangia sana uzalishaji wa gesi joto kwa sababu asilimia zaidi ya 98 ya mahitaji ya

usafiri wote wa umma hutolewa na daladala ambazo nyingi zina zaidi ya miaka 10 na hazitunzwa vizuri.

Alisema Tafiti zilizofanywa zimeonyesha kwamba kuanzishwa

kwa mfumo wa BRT awamu ya kwanza, umepunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa gesi chafu ya ukaa, ambapo kwa mabasi 210 ambayo yamekuwepo, yamepunguza uzalishaji wa gesi chafu ya ukaa kwa tani 1,616.84 kwa mwaka kwa kuondoa dadalada 11,000 kwenye ushoroba wa BRT awamu ya kwanza.

Msigwa alitumia mkutano huo wa kwanza tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo naMsemaji Mkuu wa Serikali kumshukuru Mhe Rais kwa kuendelea kumuamini ambapo pia aliwashukuru waandishi wa habari kwa jinsi wanavyoshirikiana na Serikali kwa mambo mbalimbali.

Mkutano wa namna hiyo kwa awamu inayofuata utafanyika Mkoa wa Morogoro na Dodoma.

 

No comments:

Post a Comment