NA MWANDISHI WETU, MONDULI
TAASISI ya Wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni(MAIPAC), imepongezwa na wananchi wa Kijiji cha Selela, wilaya ya Monduli kwa kukamilisha mradi ya ujenzi wa uzio kulinda chanzo cha maji ya Kabambe, kilichopo Kata ya Selela, wilaya ya Monduli, mkoa Arusha.
Chanzo hicho cha maji, kilikuwa hatarini kutoweka, kutokana na ongezeko la shughuli za kibinaadamu na kuharibiwa na mifugo na Wanyamapori.
Wakizungumza wakati wakikagua mradi huo, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma na meneja miradi, Andrea Ngobole, walieleza kuridhishwa na ujenzi wa uzio huo, wenye urefu wa zaidi ya mita 700.
Juma alisema mradi huo ulianza rasmi mwezi Julai mwaka jana ni sehemu ya mradi uliotekelezwa na MAIPAC kwa ufadhili wa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania chini ya uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.
MAIPAC pia inaendelea na mradi wa kukusanya taarifa za maarifa ya asili ya jamii za Wahadzabe, Datoga na Maasai na katika uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Tunashukuru serikali ya kijiji cha Selela na kamati ya mazingira na wananchi wa Selela kwa ushirikiano mkubwa ambao wametoa hadi kukamilika kwa mradi huu” Alisema
Awali Meneja Miradi wa MAIPAC, Ngobole alisema baada ya mradi huo, kukamilika makabidhiano rasmi yatafanyika, baada ya serikali ya Kijiji cha Selela kukamilisha kuunda kamati mpya ya mazingira ya Kijiji.
“tutafanya makabidhiano rasmi ya mradi huo, kwa serikali ya Kijiji kupitia kamati ya mazingira ili mradi huu, utunzwe na Kijiji na kuendelea kuwa chini ya usimamizi wa kamati ya mazingira ya Kijiji”alisema Ngobole.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Selela,Longidonyi Lunda alipongeza taasisi ya MAIPAC kwa kukamilisha mradi huo na kuomba taasisi hiyo, kuendelea kusaidia shughuli za maendeleo katika Kijiji hicho.
“Bado tunaomba mtusaidie kukarabati bomba za maji ambazo ziliharibiwa na mafuriko lakini pia kusaidia akina mama kuwa na mradi wa kujipatia kipato”alisema mwenyekiti huyo
Mkandarasi wa mradi huo, Ephrahimu Samweli alisema mradi huo, utakuwa na manufaa kwa jamii kwa muda mrefu kwani sasa mifugo na wanyamapori haiwezi kufikia maeneo ya chanzo cha maji.
“Hivi sasa hata watu kuingia ndani ya chanzo cha maji ni mpaka kupata ruhusa kwa viongozi kufunguliwa geti hivyo, chanzo kitakuwa salama sana kwa muda mrefu na inategemewa maji kuongezeka sana”sana.
No comments:
Post a Comment