NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameisifu taasisi inayojihusisha na mpango wa kukuza kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania ( SAGCOT) kwa kuwa mfano wa kuigwa katika maendeleo ya kilimo hapa nchini ambapo kupitia utendaji kazi mzuri wa taasisi hiyo, amesema kuwa Serikali imeamua kuanzisha Mpango wa Kukuza Kilimo nchini ( AGCOT) wenye lengo la kukuza kilimo hapa nchini kwa kuanzisha kanda nyingine tatu za kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima hapa nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa AGCOT uliohudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo Hussen Bashe, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa SAGCOT imekuwa mfano wa kuigwa katika kipindi cha miaka 14 iliyopita tangu kuanzishwa kwake kwa kuendeleza kilimo katika Kanda ya Kusini.
“Kama Serikali, tunajivunia mafaniko haya ya SAGCOT ya kuendeleza kilimo katika Ukanda wa Kusini na mpango huu tayari umeonesha mafanikio makubwa,”
“Kupitia mafanikio haya, Serikali katika mwaka wa fedha 2022-2023 tuliamua kutanua wigo wa SAGCOT na kuanzisha kanda nyingine tatu mpya chini ya mpango huu, ili kufikia wakulima wa maeneo mengine hapa nchini, kuongeza uzalishaji wa mazao na kunyanyua hali zao za kiuchumi ,” amesema Majaliwa.
Ukanda wa Kusini ambao umepata mafanikio chini ya usimamizi wa SAGCOT unajumuisha mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Dar es Salaam na Pwani.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa kutokana na mafanikio ya kilimo katika ukanda huo, Serikali imeamua kuanzisha kanda nyingine mpya , hatua ambayo inalenga kuongeza uzalishaji wa mazao na ufanishi katika sekta ya kilimo kwa kutumia mbinu shirikishi zinazozingatia hali halisi ya kijiografia na ikolojia ya maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amezitaja Kanda tatu mpya zilizoanzishwa kuwa ni Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.
Kanda nyingine ni ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma huku Kanda ya tatu ikiwa ni ya Ziwa na Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Mara na Kagera.
Amesema kuwa Serikali inataka kuona kanda hizi mpya zinaiga mafanikio yaliyopatikana katika Kanda ya Kusini inayosimamiwa na SAGCOT.
“Lengo ni kuhakikisha kila eneo la kilimo linapangwa na kuendelezwa kwa kulingana na hali ya hewa, aina ya udongo inayopatikana katika eneo husika na kuzingatia sifa nyingine zikiwemo za kijiografia,” amesema Majaliwa.
Amesema kupitia mpango huu, wananchi watafahamu aina ya mazao yanayofaa kulimwa katika maeneo yao, kuongeza uzalishaji na kupunguza hasara zinazotokana na kilimo kwa kutokuwa na taarifa sahihi.
Ameongeza kuwa ili kuleta tija, kila kanda itakuwa na ratiba ya kipekee ya upandaji mazao na kuwa na wakulima kupewa taarifa ya mazao gani yanaweza kustawi zaidi katika maeneo yao na sababu za kijiografia za maeneo husika ndio zitakazozingatiwa katika mpango huu.
No comments:
Post a Comment