WIZARA ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA KILIMO KUZALISHA MBEGU BORA: NJOHOLE - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, July 29, 2025

WIZARA ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA KILIMO KUZALISHA MBEGU BORA: NJOHOLE


MWANDISHI WETU


WIZARA ya Kilimo itaendelea kushirikiana na wadau wa kilimo ikolojia na wakulima, ili kuzalisha mbegu bora na salama.


Kauli hiyo imetolewa na Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Mbegu za Mimea, Twalib Njohole akifungua warsha ya siku tatu, kuhusu uzoefu juu ya nafasi ya mbegu za wakulima katika miongozo ya kisera.


Warsha hiyo inashirikisha wadau wa mbegu za wakulima kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Senegal, Malawi, Uswisi, Zambia, Zimbabwe, Ethiopia na Umoja wa Ulaya (EU).



Njohole alisema juzi kuwa Serikali inatambua umuhimu wa mbegu za wakulima, hivyo watatoa ushirikiano wa kila aina ili kuhakikisha zinazalishwa kwa wingi.



Alisema Wizara imewezesha makundi ya wakulima, kuzalisha mbegu bora zinazokubalika sokoni.Pia wanatoa mafunzo kwa wataalamu wa kilimo wa wilaya, kwa kushirikiana na wadau kuhusu sera na kuwezesha taasisi za Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Uthibiti wa Mbegu Tanzania (TOSCI) na Wakala ya Mbegu za Kilimo (ASA).


Njohole alisema kipaumbele kwa Wizara, ni kuhakikisha mbegu bora zinazalishwa ili kuongeza uzalishaji.




Alisema pamoja na uzalishaji mbegu bora na nyingi, pia wanazingatia mbegu hizo kupatikana kwa wakati akiongeza kuwa warsha hiyo ni muhimu kwa maslahi ya sekta ya kilimo, hasa mbegu.



Mratibu wa Mtandao wa Baionuwai Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi alisema wameandaa warsha hiyo ili wadau wajadili mbegu za wakulima.


Alisema kilimo nchini kinapitia changamoto kama za mabadiliko ya tabianchi, hivyo mbegu ni mkombozi.Mratibu huyo alisema wamekuwa wakiwajengea uwezo wakulima ili mifumo ya chakula iwepo na iwe endelevu.




Mkindi alisema kwa sasa Tanzania kuna benki zaidi ya 30 za mbegu, hali inayotoa matumaini kuwa siku moja jamii itageukia kilimo cha matumizi ya mbegu za wakulima.


Mwakilishi Mkazi wa Shirika la SWISSAID Tanzania, Betty Malaki alisema mbegu za wakulima zimethibitisha bila shaka, kuwa ni safi na salama kwa watumiaji na mazingira kwa ujumla.


Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Islands of Peace (IDP), Ayesiga Buberwa alisema kwa siku za karibuni, wamekuwa wakipata ushirikiano wa Serikali katika eneo la mbegu za wakulima, zenye mchango mkubwa kwenye kilimo.




Alishukuru Serikali kwa kuthibitisha aina 17 za mbegu za wakulima jambo linalowapa nguvu kusukuma gurudumu hilo.




Alisema juhudi za kuendeleza mbegu za wakulima, zitaonekana zaidi kupitia uamuzi wa Serikali kuzithibitisha kwa matumizi rasmi.


Dk Atugonza Bilaro wa TARI, alisema mbegu za wakulima ni bora, hivyo kutaka wadau waweke mkazo ili zitambulike kisheria na kisera.


No comments:

Post a Comment