WANAWAKE FANI YA SAYANSI, TEKNOLOJIA, UHANDISI NA HISABATI WASISITIZWA KULINDA BUNIFU ZAO. - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, June 10, 2026

WANAWAKE FANI YA SAYANSI, TEKNOLOJIA, UHANDISI NA HISABATI WASISITIZWA KULINDA BUNIFU ZAO.


NA MWANDISHI WETU

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeendelea kusisitiza umuhimu wa ulinzi wa Miliki Ubunifu kupitia ushirikiano na wanawake wa fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati hatua inayolenga kuongeza uelewa kuhusu haki za Miliki Ubunifu ili kuhakikisha bunifu za watanzania zinalindwa, zinathaminiwa na zinachangia kikamilifu katika maendeleo ya jamii na kutatua changamoto zilizoizunguka jamii kwenye maisha yao ya kila siku.


Hayo yamebainishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa leo tarehe 09 Juni 2026 wakati akifungua warsha ya Miliki Ubunifu kwa wanawake katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi pamoja na Hisabati (STEM) iliyofanyika katika ukumbi wa Tume ya Ushindani jijini Dar es salaam.


Akizungumza katika hotuba yake,  Nyaisa alisema kuwa warsha hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa mkakati wa BRELA kuwafikia wabunifu waka kada na fani zote ili kuwaelezea umuhimu wa ulinzi na ubiasharishaji wa bunifu zao.


“Kwa kutambua umuhimu wa fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati katika uvumbuzi BRELA imeona ni vyema kuandaa warsha hii ili kuwapa ninyi nafasi ya kujifunza masuala ya Miliki Ubunifu pamoja na urasimishaji wa biashara zinazotokana na bunifu mnazozifanya,” alisema Bw. Nyaisa.


Awali akimkaribisha Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa, Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu, Seka Kasera alisema idadi ya wanawake katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uandisi na Hisabati kwa sasa imezidi kuongezeka na kwamba warsha hiyo itasaidia wanawake wengi kwenye fani ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati kulinda bunifu zao.


Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa warsha hiyo walieleza kuwa warsha hiyo imebadilisha kwa kiasi kikubwa mtazamo wao kuhusu masuala ya Miliki Ubunifu hasa kwenye kulinda kazi ambazo wanabuni kwenye kada yao ya STEM.


“Temekuwa tukitengeneza bunifu mbalimbali na tunaishi nazo, unakuta mwingine hajasajili popote wala kulinda bunifu yake ambayo inamsaidia kutambulika, mtu anaweza akabuni leo na mtu mwingine akaja akabuni kitu kinachofanana na chako na akakisajili na wewe ukakosa mahali pakwenda kulalamika hata kama lilikuwa wazo lako,” alieleza  Tanjana Mgonja.


Warsha hiyo yenye kauli mbiu isemayo ‘Bunifu zetu, Nguvu yetu kwa Maendeleo ya Jamii na Taifa Letu’ imewakutanisha kundi la wanawake wenye fani mbalimbali kutoka idara za Sayansi, Teknolojia, Uhandishi na Hisabati ambapo washiriki walipata fursa ya kujadili mada kuhusu Miliki Ubunifu na kutoa mapendekezo yao namna ya kuboresha bunifu zao.





No comments:

Post a Comment