Na Asha Kigundula
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic, ameanza rasmi jana kazi ya kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa kuvaana na watani wao wa jadi, Simba, mchezo utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya klabu ya Yanga zinasema kuwa kocha huyo atakuwepo katika mazoezi ya asubuhi ya leo, huku sambamba na kocha wa sasa, Sam Timbe.
Chanzo kinasema kuwa Timbe ameshapewa taarifa ya kuvunjwa kwa mkataba wake wa kukinoa kikosi hicho kwa ajili ya kumpisha kocha huyo raia wa Serbia kurudi katika nafasi hiyo.
Timbe, ambaye jana alikuwepo mazoezini hakuonesha kupata mshituko wowote kama anakiacha kikosi hicho, huku akisisitiza tu kuwa atahitaji kulipwa haki zake kutokana na mkataba alionao.
Timbe ataondoka nchini kesho baada ya kumaliza mazungumzo na viongozi wa Yanga juu ya kuvunja mkataba wake ambao ulikuwa unamalizika Mei mwakani.
Jambo Leo ilimshuhudia kocha huyo Mganda (Timbe), akiwa kwenye benchi la Yanga katika mchezo wa juzi ambapo Yanga ilicheza na JKT Oljoro na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika mazoezi ya kikosi hicho yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam, Jambo Leo lilimshuhudia Papic akianza kibarua hicho kipya ambapo atakumbana na mtihani mgumu katika mchezo wake wa kwanza msimu huu dhidi ya Simba mwishoni mwa wiki hii.
Kocha huyo ambaye aliipa Yanga ubingwa wa Kombe la Tusker mwaka jana, alikuwa 'bize' kikosi hicho ambacho amekikuta kikiwa na wachezaji baadhi wapya kwake na wale wa zamani aliowaacha, akionesha kufurahia kazi hiyo tena.
Papic anasadikiwa kurudi katika klabu hiyo kutokana na shinikizo la mdhamini anayetaka kurudi klabu hapo, Yusuph Manji, ambaye alitangaza kurudi ikiwa Yanga itakubali kumrudisha kocha huyo na aliyekuwa meneja wa timu, Emmanuel Mpangala.
Timbe alijiunga na Yanga msimu uliopita ambapo timu hiyo ilipata ubingwa wa Tanzania Bara ikiwa pamoja na Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati.
Timu hiyo inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu inayoendelea nchini, ambapo Jumamosi itavaana na Simba kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Monday, October 24, 2011
New
Papic aichukua rasmi Yanga
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment