Tatizo la Taita ni kielelezo cha wengine - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, December 19, 2011

Tatizo la Taita ni kielelezo cha wengine

Tatizo la Taita ni kielelezo cha wengine
Na Hamisi Magendela
UWEZEKANO wa kuwa na kikosi cha wachezaji wenye nidhamu na uchungu wa matokeo mabovu kwa timu yao inawezekana ikiwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakawa wakali na kusimamia adhabu zao kikamilifu.
Ukweli ni kwamba tatizo lipo kwa baadhi ya wachezaji wetu kujihusisha na masuala yasiyofaa kisoka kutokana na wao kuingia zaidi katika vishawishi kutokana na umaarufu wao.
Hivyo, hali hiyo, endapo mchezaji hatokuwa na nidhamu ya kutosha ya kuangalia kwa wakati huo, ana jukumu gani linalomkabili, anaweza kujikuta akiiweka timu katika wakati mgumu.
Inawezekana wanashindwa kuhimili mihemko ambayo kwa njia moja au nyingine inaweza kuathiri timu ya taifa na jamii kwa ujumla kwa kupoteza nguvu kazi ya taifa.
Ukiondoa kudorola kwa stamina kwa wachezaji wetu, lakini kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa magonjwa ya ngono ukiwemo ugonjwa hatari wa Ukimwi.
Pia, jambo la kukutana na makocha lisiwe kwa timu za wanaume pekee kwani hata kwenye timu za soka ya wanawake ni vyema ikaangaliwa kwa undani zaidi.
Katika siku chache zilizopita, niliweza kufuatilia mashindano ya mpira wa wanawake ya Kombe la Uhuru yaliyokuwa yakichezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam, siku za Jumamosi na Jumapili.
Nikiondoa unafiki, wachezaji wa timu zilizoshiriki mashindano hayo walionesha kiwango cha juu cha kusakata kabumbu, lakini tatizo kubwa lililoonekana ni kukosekana kwa stamina kwa wachezaji wengi.

Na Baadhi yao walionekana kumudu vyema kupiga mashuti yenye uwezo mkubwa kitu ambacho pia nakipongeza.
Baadhi yao walionekana wazi kushindwa kupiga mpira vizuri kutokana na kuonekana kutokuwa na nguvu za miguu, kitu ambacho kilisababisha kukosa mabao ya wazi.
Kila siku wachezaji hao hufanya mazoezi ya viungo kukimbia kwenye mchanga, lakini bado stamina ni tatizo, nini kinasababisha? Tukubali hao wana tatizo kubwa ambalo linapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.
Kwa upande wa akina dada, niko katika hatua za mwisho kukusanya vielelezo vya kutosha vya kubaini tatizo la stamina linatokana na nini, nikibaini nitamnong'oneza rais Tenga ili aweze kulifanyia kazi.
Tatizo lililoonekana kwa Taita linadhihirisha kuwepo kwa wachezaji wengi japo msala uliweza kumwangukia mchezaji huyo pekee kwa wakati ule, kitu ambacho hata Tenga alikiri kupata taarifa za mara kwa mara kuhusu kutoka kwa wachezaji kambini.
Tabia hiyo inawezekana kuanzia katika klabu zao wanapotoka, hivyo suala la kukutana na makocha ni la msingi kwani kuna uwezekano wa kubaini mambo mengi yatakayosaidia kujenga nidhamu kwa wachezaji wakati wote wanapoitumikia timu ya taifa na klabu zao.
Nikimnukuu kiongozi mmoja wa TFF, alisema takribani miaka 10 iliyopita, baadhi ya wachezaji wa timu moja kubwa wakiwa jijini Mwanza katika mashindano, baadhi ya wanadinga walikataliwa katakata na mmoja wa mashabiki kuingia kwenye ukumbi wa disko wakiwa na mabibi zao.
Anasema baada ya wachezaji kuwazuia kuingia kwenye ukumbi huo wa starehe, pia alithubutu kumpigia simu kiongozi wa timu hiyo kuhusu tukio hilo na wanandinga hao wakabaini hilo na kurudi haraka kambini na 'rokoo' ilipofanywa wakakutwa wametimia na kunusurika na adhabu ya kutokuwepo kambini
Hali hiyo inadhihirisha wazi vitendo hivyo havikuanza leo, na inawezekana TFF inakumbuka shuka tayari kumeshakucha, lakini bado nafasi ipo ya kufanya hivyo ili kuwa na wachezaji wenye nidhamu ambao watajenga kikosi imara wakati wote wa mashindano yao.
Wachezaji wetu wengi dakika zao ni 45 za kipindi cha kwanza, na baada ya hapo hali huwa tete, tatizo liko wapi? Nina imani hatua zinazochukuliwa na TFF zitajenga nidhamu bora kwa wachezaji kuanzia kwenye klabu zao.

0718594040

No comments:

Post a Comment